RAIS Samia Suluhu Hassan amesema anasubiri kwa hamu ripoti ya Tume ya Haki Jinai aliyoizindua jana ili aweze kupuliza zumari.
Rais Samia ameyasema hayo leo, Februari Mosi, 2023 katika kilele cha maadhimisho ya siku ya sheria nchini, yaliyofanyika kwenye viwanja vya Chinangali mjini Dodoma
Tume hiyo iliyozinduliwa na Rais jana itaongozwa na Jaji Mstaafu Othman Chande na itakuwa na jukumu kubwa la kufanya maboresho ya haki jinai ili kukidhi matakwa ya serikali na jamii ya Tanzania kwa ujumla.
Taasisi za haki jinai zitakazofanyiwa kazi na tume hiyo ni Jeshi la Polisi, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Jeshi la Magereza, na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).
Akizungumza Rais Samia amesema “Sheria zote zenye mizunguko inayochelewesha upatikanaji wa kesi zifanyiwe marekebisho, ukichelewesha kesi unachelewesha haki.
“Zumari litapulizwa nitakapopokea ripoti ya Tume, mimi ni Mpemba najua jinsi ya kuipuliza.”Amesema
|Aidha, amesema mfumo wa utoaji haki unaochelewesha ni hatari kwa nchi yetu kwa kuwa uwepo wa amani ni chachu ya manedeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
“Nchi imejengwa kwa misingi ya haki, inaweza kupotea endapo migogoro inayofikishwa mahakamani haitatuliwi kwa haraka.”Amesema Rais Samia
Amesema, mara nyingi ukiangalia migogoro inayoenda mahakamani ni kwamba haki imekosekana hivyo kutaka vyombo vya sheria kujitaidia kuimaliza haraka na kupatikana haki.
“Tujitaidi ili amani ya nchi yetu iendelee kutunzwa. Serikali tunajitaidi haki ipatikane katika mifumo yetu ndio maana jana nimezindua tume ya haki jinai. Tuwasaidie wananchi pia kujua haki zao.”Amesema
Rais Samia amesema ifike mahali watanzania wajue kufikishana mahakamani sio sawa bali kumaliza migogoro yao kwa njia ya majadiliano na usuluhishi .
Amesema kituo cha usuluhishi katika mwaka 2022 kilisajili mashauri 354, mashauri yaliyosuluhishwa kikamilifu 64 na mengine saba wamekubaliana kwa sehemu na sehemu bado hayajafikia makubaliano.
“Jambo hili ni la kutia moyo, kazi ikiendelea tutakuwa na uhakika haki itapatikana kwa haraka kupitia usuluhishi, hivyo kasi iongezeke.”Amesema.