Serikali kutovumilia wanaokwamisha mgodi nickel

MKUU wa Wilaya ya Ngara, Mathias Kahabi amesema mtu atakayejaribu kuhujumu mradi wa uchimbaji madini wa Tembo Nickel, atakuwa anaihujumu serikali jambo ambalo hatokubali litokee.

Kahabi aliyasema hayo alipokuwa akizungumza kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Rwinyana na Bugarama, alipofanya ziara  ya kuzungumza na wananchi juu ya umuhimu wa uthaminishaji mali na makazi kwa wananchi wanaozunguka eneo la mradi wa Tembo Nickel wilayani Ngara.

“Mradi huu ni mkubwa, tusiuchukulie poa, ni mradi wa kimkakati, kampuni kubwa kutoka nje ya Tanzania imewekeza pale, Tanzania tuna asilimia 16 kwenye huo mradi, mwekezaji ana asilimia 84, ni uwekezaji mkubwa utakaotufaidisha”.

“Kwa maana hiyo sisi ndo walinzi namba moja wa huu mradi, mimi kama mlinzi wa usalama ni jukumu langu kuhakikisha unafanikiwa na hakuna mtu wa kuuchezea, ukijaribu kuhujumu huu mradi ujue unaihujumu serikali na mimi sitokubali hilo litokee na Serikali ya Mkoa haitokubali,”alisema.

Alisema kuna watu wametoka maeneo mbalimbali ikiwamo Geita na Mwanza ili kurubuni wananchi wa vijiji vinavyozunguka mradi huo wawauzie maeneo yao baada ya tarehe ya katazo la kuendeleza makazi na mashamba kutolewa.

“Wamekuja wakanunua mashamba kwa fedha ndogo, tegesha ni matapeli wanataka kuvuruga uthamini, lakini wajue hizi kazi za miradi mikubwa zinafanyika kitaalamu mno, kuna picha za satelaiti zilishachukuliwa tangu Julai 18 mwaka huu, kila kilichoko shambani kinajulikana”.

“Rai yangu kwenu naomba mtoe ushirikiano kwa wathamini, wanafanya shughuli zao kitaalamu sana ili kuhakikisha kila mtu anapimiwa na kuhesabiwa mali zake na alipwe kile anachostahili,” alisema.

Alisema macho na masikio ya serikali kwa sasa yapo kwenye mradi huo wa Tembo Nickel, hivyo akawaonya viongozi wa vijiji wanaokubali kurubuniwa na wanaotaka kununua ardhi na kuendeleza maeneo yao.

“Tuna taarifa kwa viongozi wa vijiji kuingiza wahuni kwenye kamati nyeti za ardhi, tegesha wanawakatia maeneo humo, Rusumo walingia wahuni wakaathiri huko, huku hatutokubali hilo lijitokeze.

“Tunajua pia kuna wanaume walikuwa wameacha wake na watoto wakakimbia huko kwenye eneo la mradi, sasa wanarudi huko wanauza nyumba na mashamba bila kujali watoto wataenda wapi, yote hayo hatutakubali kwa sababu tunajua yatatuletea shida huko mbele,” alisema.

Mshauri Elekezi wa Mpango wa Uhamishaji watu na Makazi katika mradi wa Tembo Nickel, kutoka kampuni ya RSK, Basil Shio, alisema wanaendesha uthamini kwa kufuata sheria na taratibu za nchi na sasa hivi wamefikia asilimia 40 ya tathimini katika vijiji vinavyoguswa na mradi huo.

“Kuna maeneo hatujamaliza na kikubwa ni kwa sababu ya migogoro ya mipaka, mthamini hawezi kufanya kazi maeneo yenye migogoro.

“Kwa sasa tupo kwenye Kijiji cha Rwinyana, tulijipangia miezi minne ya kuchukua taarifa uwandani, sasa hivi tunamalizia mwezi wa pili wathamini wakiwa uwandani, na hadi sasa tupo kwenye asilimia 40, tumeshafikia wananchi zaidi ya 549 na kupima vipande vya ardhi zaidi ya 900,” alisema.

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x