Rais Samia Suluhu Hassan ashiriki kwenye mkutano wa wafanyabiashara wanawake Afrika.

Rais Samia Suluhu Hassan amelitaka Shirika Huria la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) kuwajengea uwezo wanawake na vijana kwa kuwapatia elimu ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) ili kukabiliana na soko la Afrika.

Alitoa kauli hiyo mapema Jumatatu, wakati  akifungua  kongamano la wanawake na vijana wa eneo huru la biashara la Africa litakalofanyika kwa siku tatu katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere (JNICC), Dar-es-salaam akisema Bara la Afrika linaweza kuimarika kiuchumi ikiwa ni wanawake na vijana watakuwa wataalam katika matumizi ya TEHAMA.

“Hebu tuangalie mfano huu kutoka China. Uchumi wake kupitia sayansi na teknolojia unajengwa na vijana kuanzia miaka 18-35. Kuna maprofesa wengi wenye umri wa miaka 35 ambao ni wataalam wa sayansi na teknolojia wakiongoza katika makampuni mengi ya uzalishaji…tukizingatia pia mwelekeo huo huo, Afrika tuna vijana wengi wanaoweza kujenga uchumi wetu,” Rais Samia alisema.

Rais Samia pia alisisitiza juu ya umuhimu wa kuwapatia vijana ujuzi wa namna ya kutumia rasilimali zilizopatikana katika bara hili kwa ajili ya kuongeza kipato na kukuza uchumi na amewataka vijana wa Afrika kupata elimu ya kutosha juu ya sayansi na teknolojia ili kuweza kukuza uchumi wa Africa.

Pia, rais Samia alitaja jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali yake katika kukuza na kuwawezesha wanawake na vijana nchini ambapo wamekubaliana na benki kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa wanawake na vijana.

“ Tumechukua hatua nyingine kwa kurekebisha mifumo ya kodi na tozo hivyo ili kuwapunguzia mzigo wajasiriamali wanawake na vijana, tumeanza kutoa vyeti vya viwango kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa wanaojishughulisha na usindikaji wa mazao ya kilimo. usindikaji wa madini ili waweze kukaribia soko la kimataifa,” aliongeza.

Mwisho, Rais Samia alisema kuwa serikali inalifanyia kazi suala la kuimarisha mazingira salama na rafiki ya biashara hasa kwa akina mama na  ameahidi kutatua unyanyasaji wa kibiashara unaosababishwa na wanaume wanao toa lugha mbaya kwa wanawake kwa kuhisi kuwa suala la biashara linafaa kwa wanaume peke yao.

 

Habari Zifananazo

Back to top button