Rais Ukraine kususia mkutano G20

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy amesema hatahudhuria katika kilele cha mkutano wa nchi 20 zilizoendelea kiuchumi (G20) utakaofanyika Novemba 15,2022, iwapo Rais wa Urusi, Vladimir Putin atahudhuria.

Zelenskiy aliwaambia waandishi wa habari baada ya mazungumzo mjini Kyiv na Rais wa Ugiriki kwamba amealikwa kushiriki katika mkutano wa kilele Novemba 15-16 na Rais wa Indonesia, Joko Widodo.

“Msimamo wangu binafsi na msimamo wa Ukraine ulikuwa kwamba ikiwa kiongozi wa Shirikisho la Urusi atashiriki, basi Ukraine haitashiriki. Tutaona jinsi itakavyokuwa katika siku zijazo,” alisema Zelenskyy.

Advertisement

Jana Rais wa Ukraine alisema alizungumza na Widodo kwa njia ya simu na kujadili matayarisho ya Mkutano wa G20 pamoja na mpango wa nafaka wa Bahari Nyeusi.

Urusi iliivamia Ukraine Februari 24. Vita hivi sasa katika mwezi wake wa tisa vimeua maelfu, mamilioni ya watu kuyahama makazi yao na kuharibu miji na majiji. Moscow inaelezea hatua zake kama operesheni maalum ya kijeshi.