RAIS wa Indonesia, Joko Widodo atakuwa na ziara ya siku mbili nchini Tanzania kuanzia Agosti 21 hadi Agosti 22,2023 na atapokelewa na mwenyeji wake Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu Dar es Salaam kesho.
Baada ya kupokelewa, Rais Widodo na Rais Samia watakuwa na mazungumzo ya faragha, na baadaye watakuwa na mazungumzo rasmi kuhusu ushirikiano kati ya nchi hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax amesema kuwa katika ziara hiyo imelenga kufungua maeneo saba mapya ya ushirikiano yakiwamo katika sekta za afya, nishati na madini.
Maeneo mengine yatakayotiliwa saini hati ya makubaliano ya ushirikiano ni sekta za uchumi wa buluu, ushirikiano wa kimataifa, uhamiaji na biashara.
Dk Tax amesema pamoja na kushirikiana katika harakati za ukombozi, tangu kuanzishwa ushirikiano wa kidiplomasia pamekuwepo na mafanikio makubwa katika sekta ya uwekezaji na kilimo.
Amesema kuwa hadi kufikia mwaka 2023, Indonesia imewekeza nchini miradi ipatayo mitano katika sekta za kilimo, uzalishaji wa viwandani na ujenzi.
Ameeleza kuwa mwaka 1996, Indonesia ilianzisha Kituo cha Mafunzo kwa Wakulima Vijijini (Farmers’ Agriculture and Rural Training Centre-FARTC), kilichopo Mikindo mkoani Morogoro.
‘’Kwa kuzingatia kuwa, Indonesia imepiga hatua kubwa katika kilimo cha zao la mchikichi kutokana na kuwa na mbegu bora ya zao hilo, pamoja na teknolojia ya kisasa, ziara hii itapanua wigo wa ushirikiano katika zao la mchikichi,’’ amesema.
Pia ameeleza kuwa ushirikiano huo utawawezesha wakulima wa zao hilo kunufaika na mbegu bora ya mchikichi, na hivyo kuwajengea uwezo na kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula ambayo yana soko kubwa nchini na duniani.
Dk Tax amesema kuwa Tanzania na Indonesia zina uhusiano wa muda mrefu na wa kihistoria katika nyanja za kimataifa tangu wakati wa harakati za kujikomboa kutoka katika utawala wa kikoloni kama wanachama wa Umoja wa Nchi zisizofungamana na Upande Wowote (NonAligned Movement –NAM) hivyo, nchi hizo zimekuwa zikishirikiana katika masuala mbalimbali ya kimataifa.