Rais wa kwanza JATA atunukiwa tuzo ya heshima

DAR ES SALAAM: RAIS wa kwanza wa Chama cha Judo Tanzania (JATA) Sensei Dudley Mawala ametunukiwa tuzo ya heshima ya Waziri wa Mambo ya nje wa Japani .

Sensei Dudley ametunukiwa tuzo hiyo leo Novemba Mosi, 2023 na Balozi wa Japani nchini  Yasushi Misawa,  kwa kukuza mchezo huo hapa nchini ambao ni utamaduni wa Japan

Balozi Misawa amesema tuzo hiyo ya heshima ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Japani ilianzishwa mwaka 1984 ina historia ya karibu miaka 40 na hutunukiwa watu binafsi na vikundi kwa mafanikio yao bora katika nyanja ya kimataifa kwa kutambua mchango wao katika kukuza uhusiano kati ya Japani na nchi nyingine.

Advertisement

Amesema, tuzo hiyo pia inalenga kukuza uelewano na usaidizi miongoni mwa umma wa Japani kwa shughuli za wapokeaji.

“Nikiwa Balozi wa Japan nchini Tanzania, ninayefanya kazi ya kukuza uhusiano wa Japan na Tanzania, napenda kutoa shukurani zangu za dhati na pongezi kwa Mawalla.”Amesema Misawa na kuongeza

“Bwana Mawalla amekuza utamaduni wa Kijapani, hasa Judo na Karate, katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. …; “Alikutana kwa mara ya kwanza na martial arts katika miaka ya 1970 alipokuwa bado kijana mdogo alipokuwa akisoma nchini Italia, alivutiwa zaidi na Judo, Karate na martial arts kwa ujumla,” amesema Misawa na kuongeza

“Baada ya kupata mkanda wake wa kwanza mweusi nchini Italia mwaka 1982, alirejea Tanzania na kuanza kuwafundisha Watanzania Judo na Karate katika Chuo cha YMCA Tanzania.

“Darasa lake lilikuwa na mafanikio makubwa na karibu wanafunzi 150 walifurahia kujifunza Judo.” Amesema

Mwaka 1985 Dudley alianzisha Chama cha Martial Arts Tanzania, ambacho baadaye kilikuja kuwa Chama cha Karate Tanzania na Chama cha Judo Tanzania.

“Kupitia juhudi yake, Chama cha Judo Tanzania kilisajiliwa na Baraza la Michezo la Taifa la Tanzania mwaka 1992 Judo na Karate zikapata kutambulika nchini kote Tanzania… “Judo sasa inatambulika sana nchini Tanzania.

Kwa upande wa Mawalla akizungumza ameishukuru Japan kwa kuthamini mchango wake katika Judo na kudai kuwa mchezo huo unamjenga mtu kuwa mvumilivu na mwenye nidhamu.

“Ili mtu aweze kuendelea ni lazima yeye mwenyewe awe na nidhamu ile kuangushana ni njia moja wapo ya maisha kuwa ukianguka lazima ujue una nafasi ya pili  ya kusimama na  kuendelea, judo sio mchezo wa kuumizana.”Amesema.

 

 

 

 

 

 

 

3 comments

Comments are closed.