Rais wa Namibia afariki
WINDHOEK, Namibia: RAIS wa Namibia, Hage Geingob (82) amefariki usiku wa kuamkia leo katika hospitali ya Lady Pohamba jijini Windhoek alipokuwa akipatiwa matibabu.
Akitoa taarifa kwa wananchi wa Namibia, Kaimu Rais, Dk Nangolo Mbumba amesema wanamibia washikamane na kuendeleza utulivu katika wakati huu wa maombolezo kwa mpendwa wao ambaye alikuwa akihudumu muhula wake wa pili wa urais,
“Pembeni yake, alikuwa mke wake mpendwa Madame Monica Geingos na watoto wake wakizungukwa na kikosi maalumu cha madaktari waliokuwa katika juhudi za kuokoa uhai wa Geingos,” imeeleza taarifa hiyo.
Uchunguzi wa biopsy kufuatia uchunguzi wa kawaida wa matibabu mnamo Januari ulibainisha mpendwa huyo kuugua ‘saratani ya seli’, ofisi ya Geingob ilisema wakati huo.
Geingob alikuwa Waziri Mkuu aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi wa Namibia na Rais wa tatu wa taifa hilo, amehudumu tangu aliposhinda Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2014 na kuapishwa Machi 2015.
“Taifa la Namibia limepoteza mtumishi mashuhuri wa watu, kigogo wa mapambano ya ukombozi, mbunifu mkuu wa katiba yetu na nguzo ya nyumba ya Namibia,” amesema Mbumba.
Amesema Baraza la Mawaziri litakutana mara moja kufanya mipango muhimu ya serikali.
Alizaliwa katika kijiji kaskazini mwa Namibia mwaka wa 1941, Geingob alikuwa rais wa kwanza wa nchi ya kusini mwa Afrika nje ya kabila la Ovambo, ambalo linaunda zaidi ya nusu ya wakazi wa nchi hiyo.
Amekuwa mwanaharakati dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini, ambao wakati huo ulitawala Namibia, tangu miaka yake ya awali ya masomo kabla ya kufukuzwa na kukimbilia uhamishoni.
Alikaa karibu miongo mitatu nchini Botswana na Marekani.
Namibia itaandaa uchaguzi wa rais na bunge la kitaifa kuelekea mwishoni mwa mwaka.