Ramaphosa agoma kujiuzulu
Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amesema hatojiuzulu licha ya mashinikizo mbalimbali yanayomhusisha na kashfa ya ufisadi ambayo hata hivyo alikanusha kutohusika dhidi ya kashfa hizo.
Msemaji wa rais huyo, Vincent Magwenya amewaambia waandishi wa habari jana kuwa Ramaphosa hatajiuzulu kwa kutegemea ripoti ya ufisadi dhidi yake ambayo aliita yenye dosari.
Magwenya amesema rais huyo ataka rufaa dhidi ya ripoti hiyo kwa maslahi ya muda mrefu na kwa lengo la kulinda demokrasia endelevu ya kikatiba nchini humo.
Ramaphosa anakabiliwa na shutuma mbalimbali zinazomtaka ajiuzulu baada ya uchunguzi wa Bunge kubaini kuwa huweda alikiuka sheria za kupambana na ufisadi kuhusiana na wizi wa mamilioni ya Dola katika shamba lake la Phala Phala.
Kamati ya uchunguzi ya Bunge la Afrika Kusini iliibua maswali katika ripoti yake kuhusu chanzo cha fedha hizo za Cyril Ramaphosa na kwa nini kiasi chote hicho hakikutangazwa kwa mamlaka husika za fedha.
Ramaphosa amekanusha tuhuma hizo na kusema kuwa pes hizo alizipata kutokana na mauzo ya wanyama wa shambani kwake. Wakati huo huo, vyama vya upinzani na wapinzani wa Ramaphosa ndani ya chama tawala cha ANC vimetoa wito wa kujiuzulu kiongozi huyo.
Wanachama wa ANC wanatazamiwa kukutana leo katika mkutano wa Kamati Maalumu ya Kitaifa ya Kazi kujadili kadhia ya Ramaphosa. Baada ya kikao cha leo, Kamati Kuu ya Taifa ya chama hicho kinatazamiwa kukutana hapo kesho kuamua juu ya hatua itakayomchukuliwa Rais huyo wa Afrika Kusini.