Mkurugenzi Mkuu Msaidizi na Mkuu wa Kitengo cha Kusini mwa Jangwa la Sahara wa Shirika
la Maendeleo na Ushirikiano la Uswisi (SDC), Balozi Nicolas Randin, alifanya ziara ya kikazi
nchini Desemba 3-8, mwaka huu.
Ziara hiyo ilikuwa na lengo la kukagua miradi inayofadhiliwa na Serikali ya Uswizi nchini Tanzania na kukutana na washirika wa miradi hiyo.
Katika ziara yake, Mkurugenzi Msaidizi alikutana na wawakilishi wa asasi za kiraia, maafisa wa miradi,
viongozi wa serikali na wadau wa maendeleo.
Ziara hiyo pia ilijumuisha kutembelea miradi inayofadhiliwa na Uswisi katika Mikoa ya Dodoma, Morogoro na Pwani. Balozi Randin aliambatana na Mkuu wa Kitengo cha Mashariki na Kusini mwa Afrika cha SDC Bi. Katharina Stocker na Mkuu wa Kitengo cha Amani, Utawala na Usawa cha SDC, Christine Schneeberger.
Mnamo Desemba 4, mwaka huu, ujumbe ulifanya mkutano na wadau kutoka kwenye miradi ya vyombo vya
habari, kupambana na rushwa na asasi za kiraia. Katika mkutano huo, wadau walitoa maoni yao juu
ya muktadha wa kisiasa na jukumu la Asasi za Kiraia nchini.
Ujumbe huo ulitembelea mradi wa TASAF katika Kijiji cha Ruvu Darajani Chalinze na kufanya mazungumzo na
baadhi ya wanufaika wa mradi huo.
Wakiwa Dodoma, walikutana na wanufaika wa mradi wa ‘Safeguard Young People (SYP)’ na walipata nafasi ya kuzungumza na kina mama vijana ambao wamepata ujuzi wa maisha, afya ya uzazi, uongozi na ujasiriamali.
Ujumbe huo pia ulitembelea Chuo cha Maendeleo ya Wananchi cha Morogoro kinachofadhiliwa na
mradi wa Skills for Employment Tanzania (SET); ulitembelea Taasisi ya Afya Ifakara (Ifakara Health
Institute) iliyopo Bagamoyo na Kilimo Fresh. Sehemu zote hizo zinatekeleza miradi inayofadhiliwa na
Serikali ya Uswisi.
Uswisi imefadhili miradi mbalimbali nchini Tanzania tangu mwanzoni mwa miaka ya 1960. Mwaka
1981, Tanzania ilichaguliwa rasmi kuwa miongoni mwa nchi zinazopewa kipaumbele kupata ufadhili
kutoka Uswisi. Mpango wa Ushirikiano wa Uswisi Tanzania 2021 – 2025 umejikita katika
kuwawezesha vijana hasa wanawake wasio na uwezo ili kujiendeleza kijamii na kiuchumi.
Kupitia SDC, Uswisi inaendelea kufanya kazi na washirika wake kuimarisha taasisi za serikali, kukuza nafasi
ya kiraia na kuboresha maisha ya vijana. Mwaka huu, SDC ilitenga faranga za Kiswisi milioni 24.5
kufadhili miradi ya maendeleo nchini Tanzania.
Comments are closed.