RC aagiza uzalishaji zaidi mkonge

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Omar Mgumba ameagiza Chama cha Wakulima wa Mkonge (SAT) kuja na mpango wa kuendeleza mashamba pori ili kufikia malengo ya uzalishaji wa tani 80,000 ifikapo mwaka 2025.

Kauli hiyo aliitoa jana wakati wa kikao chake na viongozi wa chama hicho cha kujitambulisha na kujua malengo ya chama hicho katika kufikia uzalishaji wenye tija.

Alisema toka serikali ilivyoweka malengo ya kuongeza uzalishaji wa zao hilo, bado nchi inazalisha tani 38,000 pekee huku mashamba pori yakiendelea kuwapo bila ya kuendelezwa.

“Serikali haikuwapa mashamba kwa ajili ya kufuga mapori wala kuyatumia kwa lengo la kupata mikopo, tulitegemea mtayatumia kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa mkonge lakini hali imekuwa tofauti, mashamba pori ndio yamekuwa mengi badala ya mkonge,” alisema.

Aliwataka kuja na mpango ambao utaonesha mikakati ya kuongeza uzalishaji lakini na changamoto ambazo zinachangia kutofikiwa kwa lengo la uzalishaji ambao utaweza kuleta tija kwao na serikali kwa ujumla.

Alisema kutokana na mkonge kuwa miongoni mwa mazao ya kimkakati nchini, ni muhimu wadau wa zao hilo na serikali wakaweka nguvu za pamoja kufikia lengo.

Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Mkonge, Saad Kambona alisema serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri ya matumizi ya bidhaa za mkonge ili kukuza soko la ndani.

Alisema baadhi ya miongozo ya kudhibiti matumizi ya kamba za plastiki imeweza kutolewa sambamba na matumizi ya vifungashio vinavyotokana na mkonge ili kuimarisha soko la ndani la bidhaa hizo.

Mwenyekiti wa chama hicho, Robert Semwaiko aliiomba serikali kuwasaidia kupata masoko yenye uhakika wa zao hilo kutokana na wananchi wengi kuhamasika kulima.

Aliomba pia serikali kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja katika maeneo ya kwenye mashamba ili kurahisisha usafirishaji wa zao hilo kwenda kwenye mashine za uchakataji.

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button