MKUU wa Mkoa wa Arusha, John Mongella amewataka vijana kukabili changamoto zilizopo katika kilimo ili kujikwamua kiuchumi.
Aidha, alisema ingawa kilimo si kitu rahisi ni ajira na uhai hivyo lazima vijana wahakikishe wanapambana na mazingira ili waweze kufanikiwa.
Mongella alisema hayo wakati wa uzinduzi wa Programu ya Vijana na Samia Tuijenge Tanzania na anayeamua kulima, kilimo kinalipa.
Alisema Rais ameelekeza kila mkoa kutoa nafasi ya ajira kwa vijana hivyo anaamini maelekezo hayo yatajenga vijana katika kuhakikisha vijana wanajikwamua kiuchumi kupitia kilimo.
“Kilimo ni ajira na lazima mjue kilimo sio mchezo, ukiamua kuwekeza unajikwamua kiuchumi,” alisema Mongella.
Naye kijana mkulima, Sesani Msafiri alisema vijana waliokutana hapo wapo tayari kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika kampeni ya “Vijana Twendezetu Shamba, Mama Kamwaga Mkwanja”.
Aliomba serikali ipunguze kodi zinazokatisha tamaa wakulima katika kuboresha mazao na kuomba mazao yatakayozalishwa na vijana hao ya kimkakati yanuifaishe vijana waliojitokeza.
“Mikopo isiwe ya juu sana kwa vijana ili waweze kukopa na kuingia shambani kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi,” alisema Msafiri.
Awali Frank Festo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kampeni ya Vijana Twenzetu Shamba, Mama Kamwaga Mkwanja aliishukuru Taasisi ya Mwalimu Nyerere kwa kuhakikisha mradi huo wa vijana Twenzetu Shamba unawanufaisha vijana zaidi kwa kulima mazao ya kimkakati.
Sh bilioni 954 zimetengwa kwa ajili ya kuwawezesha vijana kulima ikiwemo kupata hati ya mashamba yao na kutengeneza skimu za umwagiliaji hadi kutafutiwa masoko nje ya nchi.
“Rais ni mpole na anaona vijana wanashida na mashamba, hawana ajira hivyo kutokana na tatizo la ajira kwa vijana na ameamua kuwawezesha vijana kupata mashamba kwa kujenga uchumi shirikishi kwa walionacho na wasionacho,” alisema.
Vijana milioni 3 wanatarajiwa kufikiwa na mradi huo wa Twenzetu Shamba, Mama Kamwaga Mkwanja.