BARIADI, Simiyu: MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahaya Nawanda amesema wamebaini uwepo wa zaidi ya ekari hewa 170,000 za mashamba ya pamba baada ya kuanza kufanya uhakiki kwa wakulima.
Nawanda alisema kuwa uhakiki huo ulifanyika katika wilaya zote tano za mkoa huo na kuwa awali wakulima walidanganya na kuchukua viuatilifu (sumu za kuua wadudu) wakidai wana ekari hizo.
Alisema hayo jana wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyabiashara Mkoa, ambacho kilifanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu huyo wa Mkoa na kuongeza kuwa katika Wilaya ya Bariadi ekari hewa zilikuwa 40,000, Maswa 30,000, Busega 23,000, Itilima 28,000 na Wilaya ya Meatu ekari hewa zilikuwa 60,000, jumla ni hekari hewa 175,000 mkoa mzima.
“Hizi ekari wakulima wake walidanganya na kuchukua viuatilifu, watu wamekuwa wakidanganya lengo likiwa ni kuchukua hizo sumu za kuua wadudu ili wakauze, mtu anasema ana ekari 20, kwenye uhakiki tumekuta ana ekari mbili,” alisema.
Dk Nawanda alisema kuwa katika msimu ujao wa kilimo cha zao hilo, uhakiki wa mashamba utafanyika mapema na kila mkulima ataonesha shamba lake na kupigwa picha. Katika kikao hicho wafanyabiashara waliomba serikali kuingilia kati changamoto ya ulipwaji wa madeni yao ambayo wanadai katika halmashauri za mkoa huo kutokana na kukaa muda mrefu bila kulipwa.
“Kuna madeni hapa wafanyabiashara tunadai toka mwaka 2004 baada ya kutoa huduma kwenye hizo halmashauri, lakini mpaka sasa hatujalipwa, tumekuwa tukihangaika na tumekutana na ugumu wa kulipwa madeni hayo,” alisema Christopher Muhama.
Mratibu wa Mabaraza ya Wilaya na Mikoa kutoka Baraza la Biashara Taifa (TNBC), Marco Chacha akizungumza wakati wa kikao hicho alisema, Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye mwenyekiti wa baraza hilo taifa atatoa zawadi kwa baraza la mkoa, wilaya na wizara ambalo litafanya vizuri katika utekelezaji wa majukumu yake.