RC aipigia chapuo Self Microfinance kwa kukuza mitaji

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Omari Mgumba ameupongeza Mfuko wa Self Microfinance kwa kukuza mitaji yao kutoka Sh bilioni 57 mwaka  2016 hadi kufikia Sh bilioni 59.8 Juni 2022, jambo ambalo ni muhimu kwa ustawi wake.

Mgumba aliyasema hayo  wakati akifungua matawi manne ya mfuko huo.

Alisema amefarijika zaidi kwa mpango mkakati wa kuhakikisha wanaongeza matawi ili kufika mikoa yote ikiwemo kufarijika kuona mfuko huo unafanya kazi nchi nzima Tanzania bara  na Zanzibar.

Alisema serikali inafahamu mfuko huo ni moja ya taasisi muhimu ya fedha katika maendeleo ya sekta ya fedha na uchumi na kichocheo cha uchumi na ustawi wa maendeleo ya uchumi katika nchi.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kwa kipindi kilichoishia Desemba mwaka 2020/2021 mchango wa sekta ya fedha na bima katika pato la taifa ulikuwa kwa asilimia 10.

“Utoaji wa  mikopo kwa sekta binafsi ulikuwa kwa asilimia 10 ukilinganishwa kwa ukuaji asilimia 3.1 mwaka 2020 na hiyo ni rejea hali ya uchumi mwaka 2022, hivyo kuendelea kuchochea shughuli za kiuchumi kakika mfuko umechangia kwenye ukuaji huo kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya mfuko huo, Paul Sangawe alitoa shukrani kwa Rais Samia kwa imani kubwa ambayo  aliionesha kwao kuweza kuwakabidhi jukumu hilo la kusimamia utekelezaji wa majukumu hayo huku akiahidi wataendelea kusogeza huduma karibu na wananchi.

Alisema kwa kipindi kifupi mfuko umekuwa hadi kufikia kuwa na matawi 12 hapa nchini, malengo ni kufikisha huduma karibu katika maeneo yote hapa nchini.

 

Habari Zifananazo

Back to top button