RC akagua miradi Kongwa

RC akagua miradi Kongwa

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amefanya ziara wilayani Kongwa iliyohusisha kukagua mradi wa maji pamoja na wa kituo cha afya katika Kata ya Mkoka.

Kituo cha Afya Mkoka kilipokea Sh milioni 300 katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya kujenga majengo mbalimbali ambapo imeelezwa kwamba jengo la wazazi na jengo la upasuaji yamekamilika kwa asilimia 97.

Lakini ujenzi wa maabara ilielezwa kwamba utakamilishwa awamu nyingine ya fedha.

Advertisement

Mkuu wa mkoa aliambiwa kwamba pamoja na hatua iliyofikiwa, mradi umekuwa ukikabiliana na changamoto ya mfumuko wa bei na hivyo wazabuni kukataa kuleta vifaa.

Akizungumzia Mradi wa Maji wa Kijiji cha Mkoka, Jumanne Selemani kutoka Kampuni ya Mashauri Trading alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa katika mradi huo wa Sh milioni 681.5 tayari wameshajenga nyumba ya pampu na kuweka tangi lenye ujazo wa lita 50,000.

Alisema pia wamejenga kisima chenye urefu wa mita 20.3 na kwamba ulazaji wa mabomba unaendelea.

Alisema wamepanga pia kukarabati tangi la zamani ili litumike na kwamba ukarabati huo utawanufaisha wananchi 10,918 pamoja na mifugo yao kupata maji.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa ya kituo cha afya na mradi wa maji, Senyamule alisema lengo la miradi hiyo ni kuwafikishia karibu wananchi huduma ya afya na maji.

Kwa upande wa afya alisema wanakijiji cha Mkoka wamekuwa wakilazimika kutembea umbali wa kilomita 45 ili kuifuata.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Remidius Emmanuel alisema Wilaya ya Kongwa ni eneo la kihistoria kutokana na wapigania uhuru wengi wa nchi za Kusini mwa Afrika kuishi hapo.

Kutokana na hilo alisema Kongwa imekuwa ikipata wageni wengi wanaokuja kutembelea eneo hilo la kihistoria, hali inayoifanya wilaya kuwa na mkakati wa kuboresha maeneo ya kihistoria ili baadaye yawe chanzo cha mapato.

Mkurugenzi wa Halmshauri ya Wilaya ya Kongwa, Dk Omary Nkullo alimweleza mkuu wa mkoa kuwa ujenzi wa madarasa ya fedha za ahueni ya Covid-19 umekamilika na kwamba kwa kutumia fedha hizo wameweza kujenga na kuanzisha shule mpya saba.

Dk Nkullo alimweleza mkuu wa mkoa kuwa wanaendelea kuvisha ng’ombe hereni na kusimamia miradi ya afya iliyofadhiliwa na Serikali ya Korea Kusini pamoja na mradi wa kudhibiti sumu kuvu, mradi wenye thamani ya Sh bilioni 99 unaofanyika katika eneo la Mtanana ambao bado unaendelea.

Katibu Tawala Mkoa wa Dododma, Dk Fatma Mganga, alisema Halmashauri ya Kongwa ina changamoto ya watoto kuacha shule ambapo watoto 4,419 wameacha shule wakiwa darasa la nne.

Kwa upande wa sekondari alisema asilimia 26 ya wanafunzi ni watoro na kwa kidato cha nne wanafunzi 492, sawa na asilimia 11.3 hawajafanya mtihani wa majaribio wa moko.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa aliwapongeza Kongwa kwa kazi nzuri ya sensa na mapokezi ya mwenge.

Aliwataka pia viongozi Kongwa kuongeza nguvu na kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kuvalisha hereni mifugo.

“Kuhusu masuala ya kuandikisha wakulima kwa ajili ya ruzuku ya mbolea na masuala ya kilimo ni vyema wananchi wakaelezwa umuhimu wa kutumia majina yaliyopo kwenye kitambulisho cha NIDA na cha mpigakura kwani hii itapunguza changamoto ya utofauti wa majina,” alisema.

 

 

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *