MKUU wa Mkoa wa Arusha, John Mongella amehoji aliyewaroga Jiji la Arusha kwa vile kila ujenzi unaojengwa fedha hazitoshi na wanaomba nyingine.
Mongella amesema hayo wakati wa kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu Hesabu za Serikali (CAG), ambapo Jiji la Arusha imepata hati ya mashaka.
Amesema miradi mingine ina shida, inajengwa mara mbili ya fedha na kuagiza kuanzia sasa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Juma Hamsini asimamie miradi inayojengwa na kwamba fedha zilizotengwa ndio zitamaliza mradi husika.
“Nani amewaroga nyie Jiji la Arusha, nataka kuwaambia kuanzia sasa hakuna kuongeza fedha katika miradi ambayo imeshatolewa fedha tayari, hapa kuna siasa nyingi, lakini Mkurugenzi nakuacha uangalie kwanza Jiji linavyoenda halafu tutaelewana vizuri hili Jiji lina vituko vyake, sasa tumesema basi, ” amesema.
Amewataka madiwani wa Jiji hilo kumpa ushirikiano Mkurugenzi Hamsini na kuachana na siasa zisizo na tija, badala yake waungane kwa pamoja kwa aajili ya kuleta maendeleo.