RC asitisha kupokea taarifa ya migodi

MKUU wa Mkoa wa Mara, Suleiman Mzee amesitisha kupokea taarifa ya migodi ya madini iliyo mkoani humo, mpaka baada ya ziara katika migodi hiyo inayolenga kumjengea mazingira mazuri ya kupokea taarifa hiyo.

Alieleza hayo wakati akizungumza na wachimbaji wadogo 387 wazawa wanaounda mgodi wa dhahabu wa Isaranilo, Buhemba mkoani humo baada ya kutembelea mgodi mwingine wa dhahabu wa ZEM jana, wenye leseni ya uchimbaji wa kati.

Alipongeza wachimbaji hao kwa kuungana, kuanzisha mgodi huo na kujenga Jengo la Soko la Madini mabalo limefikia hatua za kumaliziwa likiwa limegharimu Sh milioni 375, baadhi ya maeneo yakiwa yameanza kutumika.

“Sasa mmalizie na mzingatie kuweka maduka na vitu vingine muhimu nilivyowashauri ili mpate huduma muhimu kwa urahisi,” alisema.

Pia alikataza uchomaji wa awali wa dhahabu kwa kutumia mkaa kwa kuwa pamoja na mambo mengine ni kinyume na uhifadhi wa mazingira. Aliagiza itumike njia nyingine bora na salama zaidi.

Mzee aliagiza umoja huo kuboresha makazi na mazingira wanayoishi kwa sababu ni miongoni mwa mambo yanayoweza kudhoofisha au kuboresha afya zao.

Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Moses Kaegele alisema wachimbaji hao wamekuwa miongoni mwa vyanzo vikuu vya mapato ya halmashauri hiyo, kwamba hutoa mapato kati ya Sh milioni tatu hadi nne kwa wiki.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wachimbaji waliomba kuwekewa mfumo mzuri wa kulipa tozo tofauti za serikali ili watunze na kukuza mitaji yao.

Mmoja wao, Samwel Ojoro alitaka wajengewe hospitali kubwa na shule bora zisizopungua tatu, kwamba eneo hilo lina wakazi wengi ambao wanastahili huduma bora za kijamii.

Mchimbaji mwingine, Tumsifu Yusufu alitaka zinapobuniwa tozo mpya, elimu itolewe kwa wananchi ili kuwe na uelewa wa pamoja na hivyo kuwepo utayari wa kulipa tozo husika bila usumbufu.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button