MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema wakazi wa Dodoma wanatakiwa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo kama inavyofanya Dubai ambayo haina tembo na twiga lakini inaongoza kwa kupokea watalii duniani.
Akizungumza wakati wa kuwaaga wenza wa wachungaji wanaoenda kufanya utalii Ngorongoro katika Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kati jijini hapa, alisema Dodoma ni makao makuu ya nchi na ina vivutio vya ajabu ambavyo havipo maeneo mengine vinaweza kutumika kama vivutio.
Senyamule alisema wananchi wa Dodoma wanatakiwa kuanza kutangaza utalii wa makao makuu ya Serikali ambao haupo katika maeneo mengine ili watu wengine waje kuona utalii huo.
Alitaja miongoni mwa utalii huo ni mji wa serikali ambako kunajengwa maghorofa makubwa pamoja na majengo ya mahakama ambayo hayajawahi kujengwa hapa nchini tangu uhuru.
Aliwataka waanze kutangaza utalii ili watu waanze kutembelea Dodoma kuona vivituo mbalimbali ukiwemo mji wa serikali na majengo ya mahakama bora ambayo ni ya sita duniani kwa ubora, ukubwa na umaarufu wake.
Senyamule alisema Dodoma ina baraka zake inatakiwa iwe sifa ya pekee duniani, hivyo waanze kusema, “Dodoma Fahari ya Watanzania.”
Waanze kuitangaza Dodoma kama Fahari ya Watanzania, kwa kufanya hivyo watakuwa wamesaidia katika kufanya ubunifu wa kutangaza utalii wa Dodoma makao makuu ya serikali na kuhamasisha watu kufika kuona mandhari yake.
Awali, Askofu wa Dayosisi ya Central Tanganyika wa Kanisa la Anglikana Kanda ya Kati, Dickson Chilongani alisema wameandaa safari hiyo ya wenza wa wachungaji kutembelea Ngorongoro kuunga mkono juhudi za Rais Samia kukuza utalii.
Pamoja na kuunga mkono juhudi za Rais Samia kutangaza utalii pia wanaenda kufurahia mazingira kama ilivyoandikwa katika Biblia kitambo cha Mwanzo ambacho kinaonesha kwamba Mungu aliumba Bustani ya Edeni ambayo Adamu na Hawa walitembelea na kupumzika humo.
Mpango wa kutembelea mbuga ya Ngorongoro wachungaji na wenza wao utakuwa umekamilika kwa jumla ya wachungaji na wenza takribani 600 wa Dayosisi ya Central Tanganyika ambayo ina idadi kubwa ya waumini duniani kote kuwa wametembelea hifadhi hiyo.
Naye Katibu Idara ya Umoja wa Wanawake wa Kikristo (UWAKI) wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kati Dodoma, Agnes Liheri alisema idara hiyo ina wanawake wengi ambao wanafanya kazi tofauti na wameona vema kutembelea Ngorongoro.