MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ametoa wiki moja kwa wafanyabishara wote wa soko la Mwenge Coca-Cola wanaofanya biashara barabarani kurudi ndani ya soko huku akisisitiza kuwa watakaokaidi watachukuliwa hatua za kisheria.
Chalamila alifanya ziara jana katika Wilaya ya Kinondoni kwa kutembelea maeneo mbalimbali ikiwemo soko hilo na kukagua stendi ya mabasi ya Mwenge.
Alisema hayo baada ya kusikiliza malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara walioko ndani ya soko hilo wakidai wanakosa wateja kutokana na wenzao kwenda kinyume na utaratibu. Mmoja wa wafanyabiashara hao, Alvin John alisema wapo watu wachache ambao wanashirikiana na watu wasiowaaminifu ndio maana wanafanya biashara nje ya utaratibu uliowekwa.
Mwenyekiti wa soko la Mwenge, Abdallah Suleiman alieleza kuwa serikali imewapatia eneo zuri na vizimba lakini kuna wachache baadhi ya viongozi wanashawishi wafanyabiashara kukaa nje ya soko hilo.
Mfanyabiashara mwingine, Lucy Shoo alimtaka mkuu wa mkoa kufika eneo hilo wakati wa jioni na kujionea jinsi ambavyo barabara haipitiki kutokana na wingi wa wafanyabiashara.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule alisema waliamua kutumia nguvu kuwatoa na wamekuja na namna ya kupitisha mnyororo na kuweka bustani na atakayefanya biashara eneo hilo hatua zitachukuliwa ambapo kabla ya Septemba, 2023 utakamilika.