KIGOMA; SERIKALI mkoani Kigoma imeunda kamati kuchunguza kifo cha utata cha mfanyabiashara wa Katoro Wilaya ya Geita, Enos Elias ambaye ni mwenyeji wa Kijiji cha Ilabiro, Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma.
Kaimu Mkuu wa mkoa Kigoma, ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko ametoa taarifa ya kuundwa kwa kamati hiyo ya watu sita Novemba 15 mwaka huu na kuitaka kuanza kazi mara moja, huku akitoa siku saba kwa kamati hiyo kukamilisha kazi hiyo, ili taarifa hiyo iweze kufanyiwa kazi mara moja na hatua kuchukuliwa.
Marehemu Enos Elias ambaye alikamatwa na Idara ya Uhamiaji Wilaya ya Kakonko Oktoba 27 mwaka huu kwa madai ya kuwa na utata wa uraia na baadaye kuhifadhiwa kituo cha polisi Kakonko, ambapo baada ya hapo kumetokea utata wa mahali alipo hadi wiki moja baadaye ilipokutwa maiti yake ikiwa imezikwa kwenye pori la Kijiji cha Chilambo.

Wakati serikali ikitoa taarifa hiyo Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ametembelea familia ya marehemu kwenye kijiji cha Ilabiro Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma akiwa kwenye siku yake ya kwanza ya ziara ya siku nane ya kutembelea na kufanya mikutano katika majimbo yote ya mkoa Kigoma.
kizungumza na Mama mzazi wa marehemu, ndugu,familia na majirani waliojtokeza, Kabwe alisema kuwa ameongea na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni akiitaka serikali kufanya uchunguzi wa kina kubaini kilichotokea na kuchukua hatua kwa wote waliohusika na kifo hicho.
Tayari Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillius Wambura kupitia taarifa ya msemaji wa jeshi hilo, David Misime alisema kuwa polisi kwa kushirikiana na wadau wa haki jinai wameanza uchunguzi wa tukio na kutaka mtu yeyote mwenye habari na maelezo kuhusiana na kadhia hiyo kuiwasilisha kwa tume hiyo.