MKUU wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri kushirikiana na maofisa ughani kuhakiki idadi na ubora wa maghala ya vyama vya ushirika yaliyopo ili yatumike kuhifadhi mbolea msimu ujao.
Shigela amesema hayo wakati akizungumuza na wananchi wa kijiji cha Nyijundu kata ya Nyijundu wilayani Nyang’hwale mkoani Geita na kusema lengo ni kuondoa adha ya upatikanaji pembejeo kwa wakati.
Amesema uhakiki huo ukikamilika itasaidia kujua maeneo ya uhakika wa kupokea na kuhifadhi mbolea ya ruzuku kabla ya msimu wa kilimo kuanza ili adha ya waliyopata wananchi kufuata mbole umbali mrefu isijirudie tena.
Amekiri, serikali mkoani hapa inatambua changamoto ya upatikanaji wa mbole iliyojitokeza msimu wa kilimo ulioisha hivo mipango imewekwa kuhakikisha pembejeo za kilimo zinapatikana kwa wakati na ukaribu na wakulima.
“Pamba ya mwaka jana, haikuweza kuwa na ubora sana, zipo changamoto ambazo zilijitokeza, baadhi ya pembejeo hazikuja kwa wakati, na matokeo yake pamba haikuweza kustawi inavyotakiwa wilaya yetu ya Nyang’hwale.
“Nataka niwahakikishieni, serikali imeshachukua hatua, mwaka huu tunataka tulete pembejeo mapema, kama ni mbolea tulete kwenye vijiji vyetu, kama ni madawa tulete hapa, kama ni mbegu tulete kabla mvua haijanyesha.”
Aidha amewahakikishia wakazi wa Nyang’hwale kwamba serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya usafirishaji ili kutengeneza mazingira rafiki kwa wakulima kusafirisha mazao ya biashara na chakula pindi wanapovuna.
Meneja wa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) wilayani Nyang’hwale mhandisi Mapinduzi Magesa ameeleza kwa sasa wanaendelea na ukarabati wa barabara kata za Nyamtukuza na Busolwa kwa gharama ya Sh milioni 181.
Mkurugezi wa Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale, Husna Toni amekiri kupokea maelekezo ya mkuu wa mkoa na kueleza tayari wameweka mipango thabiti kuhakikisha wakulima wanapata mazingira rafiki sekta ya kilimo.