RC Geita apiga marufuku uhamisho holela watumishi

MKUU wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella amepiga marufuku uhamisho holela wa watumishi pasipo kuzingatia maslahi ya uhamisho, kwani utaratibu huo unavunja moyo utendaji wa watumishi wa umma.

Shigella amesema hay oleo wakati akizungumza na wafanyakazi katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, kwa mkoa wa Geita, ambapo alielekeza taratibu za uhamisho lazima zifuatwe.

Ameelekeza ofisi ya Katibu Tawala Mkoa kusimamia taratibu zote za uhamisho na kutoruhusu mfanyakazi yeyote kuhamishwa iwapo bajeti ya uhamisho haijatengewa, ili kuondokana na uhamisho usio na tija.

“Ni marufuku kumhamisha mfanyakazi kama bado bajeti ya uhamisho haipo, hayo ni amelekezo ya Rais, mkijua mnahamisha wafanyakazi kadhaa wekeni kwenye bajeti zenu, labda kama ameomba mwenyewe.

“Kama ana kosa amefanya anastahili adhabu suluhisho siyo kumhamisha, chukueni hatua na kumpa adhabu akiwa kwenye eneo lake kwa sababu unapomhamisha unatengeneza mzigo kwa serikali .”

Shigella ameagiza taasisi za umma na binafsi kuhakikisha wanazingatia stahiki za wafanyakazi wanapokuwa kazini kwa muda wa ziada, kwani ni matakwa ya kisheria na ni haki kwa mtumishi. 

Amekemea tabia ya wafanyakazi kutolipwa malimbikizo yao kwani inarudisha nyuma ari ya utumishi, huku akielekeza taasisi binafsi kufanya mabadiliko ya mishahara kulingana na kiwango cha serikali. 

“Niwaombe sana chama cha wafanyakazi kama hizo taasisi zipo, zinaendelea kuwanyonya wafanyakazi, kwa kuwalipa mishahara chini ya kiwango ambacho Rais wetu ameleekeza niorodhesheeni mliniletee.

“Yapo malimbikizo ya masaa ya kazi, yapo malimbikizo ya mishahara, yapo malimbikizo ya likizo, yapo malimbikizo mengi ambayo wafanyakazi wanastahili kulipwa, si tu kwa sekta ya umma, na sekta binafsi,” amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button