RC Geita awaonya walanguzi wa mazao

MKUU wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela amekemea tabia ya wanunuzi wa mazao kuwafuata wakulima mashambani na kuwataka wazingatie taratibu za biashara kwenye masoko rasmi ili kuepuka unyonyaji.

Shigella amesema hayo alipopita kukagua shamba la mkulima wa matiki maji katika kijiji cha Kafita kata ya Kafita wilayani Nyang’hwale mkoani hapa, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake wilayani humo.

Amesema wapo baadhi ya wafanyabiashara wa mazao maarufu kama ‘walanguzi’ wamekuwa na tabia ya kutumia fursa ya uelewa mdogo wa wakulima na kununua mazao yakiwa bado shambani hayajavunwa.

Ameeleza, mfumo huo wa biashara haukubaliki kwani unamunufaisha zaidi mfanyabiashara na kumnyima faida ama kumpa faida kidogo mkulima ambaye anayetegemea sekta ya kilimo kujikwamua kiuchumi.

“Wananchi wengi katika wilaya yetu ya Nyang’hwale wanalima matikiti, lakini pia wanalima mpunga, sasa mnunuzi akiwa anakuja moja kwa moja mashambani ndio mwanzo wa kumuibia mkulima.”

Amewataka wakulima kuendelea kuwa wavumilivu wakati serikali inaandaa mpango mpya wa mikopo ya halmashauri na itakapoanza kutolewa tena basi watumie fursa kwenda kukopa mikopo isiyo na riba.

Amesema hatua hiyo itasaidia siyo tu kuwapa mitaji lakini pia itawaepusha na vishawishi vya kuchukua mikopo umiza sambamba na kuuza mazao yakiwa shambani na hivo kuweza kulima kwa malengo.

Shigela amewahakikishia wakulima serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu imewekeza kwenye elimu, afya na miundombinu ili kuwasaidia kulima kisasa na kusafirisha mazao bila kikwazo.

Mkulima wa matikiti maji kijiji cha Kafita, Jeremiah Nyanda amesema kwa msimu huu wa kilimo amevuna takribani matikiti 4,000 ingawa changamoto kubwa ni upatikanaji wa mbolea na viuatirifu huko vijijini.

Amekiri ukosefu wa mitaji kwa wakulima ndio chanzo cha kuchukua mikopo umiza (mikopo yenye riba kubwa) ama kuuza mazao yakiwa shambani na hivo kushindwa kupata faida kubwa tofauti na matarajio.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale, John Izack amesema wanaendelea kuwaunga mkono wakulima kwa kuwawekea mazingira rafiki ya biashara ya mazao na kilimo chenye tija.

Habari Zifananazo

Back to top button