MKUU wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego ametoa onyo kwa wananchi wanaovamia maeneo ya hifadhi ya barabara, kuharibu alama za barabarani na kutupa taka kwenye mifereji huku akiziagiza mamlaka zinazohusika kuanza kuchukua hatua.
“Ninatoa wito kwa wananchi kuondoka na kuacha kuvamia, kuchafua au kuharibu maeneo hayo. Nawaagiza viongozi wa vijiji na mitaa watoe taarifa na kuchukua hatua,” alisema leo wakati akifungua kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Iringa.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema katika kipindi hiki cha mvua kumeanza kujitokeza uharibifu mkubwa wa barabara kutokana na kuziba kwa mifereji inayopitisha maji kunakosababishwa na shughuli za kibinadamu.
Alizitaja shughuli hizo kuwa ni pamoja na kilimo, uchimbaji mchanga na uchafuzi wa mazingira na kwamba shughuli hizo hazipaswi kuachwa ziendelee, kwani matengenezo ya barabara yanagharimu serikali fedha nyingi.
Ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zaidi ya Sh Bilioni 26.6 kwa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Iringa na zaidi ya Sh Bilioni 16. 8 kwa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura), kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya matengenezo ya barabara.
Aidha taarifa ya Meneja wa Tanroads Mkoa wa Iringa,
Mhandisi Daniel Kindole iliyotolewa katika kikao hicho inaonesha kazi ya kuhuisha taarifa za watu watakaoathiriwa na ujenzi wa barabara ya lami kutoka Iringa Mjini kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kwa lengo la kulipa fidia inaendelea.
Kindole alisema maandalizi kwa ajili ya manunuzi ya kujenga kilometa 104 za barabara hiyo yanaendelea na kwamba Mei mwaka huu mkandarasi wake anaweza kupatikana tayari kwa kuanza kazi hiyo inayofadhiliwa na Benki ya Dunia.