RC Kagera apongeza ujenzi shule Nyakahita
MKUU wa Mkoa wa Kagera Fatuma Mwasa, ameipongeza idara ya elimu Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kwa usimamizi wa miundombinu na ukamilishaji wa majengo ya Shule Shikizi ya Nyakahita, ambayo imeanza kutumika baada ya wanafunzi wa shule hiyo kutumia majengo ya tope kwa miaka kadhaa.
Mkuu huyo wa mkoa alitembelea shule hiyo itakayopokea wanafunzi wapya mwaka 2024 wapatao 720 na kutatua changamoto kubwa ya watoto wa kijiji hicho wanaotembea umbali wa kilometa 8 kufuata elimu ya msingi, huku baadhi yao wakishindwa kuendelea na masomo kutokana na umbali.
Amesema amefurahishwa kuona wanafunzi zaidi ya 200 waliokuwa wanasoma darasa la awali hadi la tatu katika shule shikizi hiyo ambayo ilikuwa na hali mbaya ya majengo ya tope na yanayovuja wakati wa mvua, sasa wanaweza kusomea katika shule nzuri na ya kisasa.
Amesema kuanzia Januari wanafunzi wote wanaotokea umbali wa kilometa nane watasoma katika shule hiyo ya karibu na hawatakuwa na mwendo mrefu.
“Nafurahi kuona leo tunaweza kuwa na madarasa mazuri mwanafunzi wa chekechea kutembea umbali wa kilometa 8 kwenda na kurudi sawa na kilometa 16 sio suala la kawaida kwa mtoto inachosha sana.
“Sasa serikali imewasikia kinachobaki ni kuhakikisha watoto wote katika Kijiji hiki wanapata haki yao ya kusoma na kuzifikia ndoto zao, ” amesema mkuu huyo wa mkoa.
Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Julius Raizer, amesema serikali imetoa kiasi cha Sh milioni 540, ambazo zimewezesha kupata vyumba vya madarasa 14,matundu ya vyoo 18 pamoja na jengo la utawala.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyakahita, Mtungi Tirutangwa amesema kuwa shule mama ina wafunzi 1765 kuanzia darasa la nne hadi la saba na shule shikizi ikiwa na wanafunzi 218 kuanzia chekechea hadi darasa la tatu, huku ufaulu wa shule hiyo ukiwa asilimia 60 katika mitihani ya kitaifa kutokana na idadi kubwa ya watoto kutembea umbali mrefu.
” Uwepo wa shule mpya utaongeza ufaulu, kwa sababu idadi ya wanafunzi hukata tamaa, kusitisha masoko na wengine wanaojitahidi kumaliza elimu ya msingi hawabahatiki kufaulu kwa sababu wanakosa masomo ya asubuhi, lakini uwepo wa shule hii ya karibu utaongeza ufaulu na kila mtoto atahitimu masomo yake,”amesema Tirutangwa.