RC Kagera ataka ufanisi wakandarasi wa maji

RC Kagera ataka ufanisi wakandarasi wa maji

MKUU wa mkoa wa Kagera, Albert Chalamila amewataka wakandarasi walioaminiwa na serikali kutekeleza miradi ya maji kuhakikisha wanatekeleza miradi hiyo kwa asilimia 100 kama mikataba inavyowaelekeza.

Aliyasema hayo wakati wa uwekaji saini na wakandarasi wanaoenda kutekeleza miradi ya maji katika vijiji mbalimbali halmashauri za Mkoa wa Kagera, ambapo Mei  mwaka huu jumla ya miradi ya maji 13 yenye thamani ya Sh bilioni 7.5 ilisainiwa  kwa ajili ya kuanza utekelezaji.

Alisema miongoni mwa mikoa iliyofanya vizuri katika utekelezaji wa miradi ya maji Kagera ilishika nafasi ya pili mwaka 2022, ambapo amesema kuwa mkandarasi ambaye atashindwa kukamilisha miradi ya maji kwa wakati ni sawa na kutia doa Mkoa wa Kagera.

Advertisement

Aliwataka kushirikiana na serikali kwani kilio kikubwa cha wananchi wa vijijini ni kupata maji safi na salama, kupunguza umbali wa kufuata maji,  hivyo aliwataka wafanye kazi usiku na mchana, ili wananchi wapate maji kwa haraka.

“Niwapongeze Ruwasa ambao wamekuwa wasimamizi wakuu wa miradi ya maji vijijini, hakikisheni mnawabana wakandarasi watekeleze miradi ya maji kwa kiwango, ili miradi hiyo iwasaidie wananchi, atakayejaribu kutukwamisha katika miradi ya maji na sisi tutamkwamisha zaidi,”alisema Chalamila.

Meneja wa Wakala wa maji na Usafi wa Mazingira Vijijini RUWASA mkoani Kagera, Mhandisi Warioba Sanya alisema ndani ya kipindi cha miaka miwili Serikali ya Awamu ya Sita imeleta kiasi cha Sh bilioni 41 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji mkoani Kagera, uchimbaji wa visima pamoja na ununuzi wa vifaa vya kusambaza maji kwa wananchi.

Alisema katika kipindi cha miaka miwili jumla ya mikataba 73 ya masuala yanayohusu maji vijijini mkoani Kagera imesainiwa, huku serikali ikiwatumia wakandarasi wa ndani katika utekelezaji wa miradi ya maji.

Alisema kuwa RUWASA itaendelea kuwasimamia wakandarasi kwa niaba ya serikali na Wizara ya Maji, hivyo miradi yote ambayo inatelezwa inakamilika kwa kiwango na inawanufaisha wananchi, ambao miaka ya nyuma walitumia muda mrefu kufuata maji kuliko  kufanya kazi za uzalishaji.