RC Katavi atoa maagizo utunzaji wa mazingira

MKUU wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, amewaagiza wakuu wa wilaya mkoani humo kuwaondoa wananchi wote waliovamia maeneo yasiyoruhusiwa kwa ajili ya shughuli za kibinadamu, ili kuendelea kutunza mazingira ya mkoa huo.

Ameyasema hayo katika hafla ya utekelezaji wa mpango mkakati wa usafi na utunzaji wa mazingira uliofanyika katika eneo la Soko Kuu Manispaa ya Mpanda.

Amewataka wananchi wa Mkoa wa Katavi, viongozi pamoja na watumishi kushirikiana vyema katika suala la utunzaji wa mazingira, ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira katika hali ya usafi.

Advertisement

Pia amewaelekeza wakuu wa Wilaya kusimamia usafi katika barabara kuu, ili kujihakikishia mifereji haizibi pamoja na miundombinu mingine kutoathirika.

“Agizo hili limetolewa na Makamu wa Rais na mimi nalisisitiza hapa, barabara kuu imekuwa ni eneo ambalo linasahaulika sana, ukipita unasafiri au unatoka kijiji kimoja kwenda kingine kule katikati ambako hakuna kijiji, kitongoji wala makazi unakuta chupa za plastiki zimejaa huko, tukila mahindi tunatupa mabunzi na majani yake na uchafu wa kila aina, mkalisimamie hilo,” amesema.

Awali akisoma taarifa ya utekelezaji  wa mpango mkakati wa usafi na utunzaji wa Mazingira Manispaa ya Mpanda, Kaimu Ofisa Afya Manispaa hiyo, Elizabeth Kakusa amesema halmashauri inaendelea kutekeleza mkakati wa Taifa wa kuhifadhi mazingira ya ardhi na vyanzo vya maji kwa kushiriki kampeni za upandaji wa miti siku ya Taifa ya kupanda miti na siku ya mazingira duniani.

“Hii ni kuhakikisha lengo la kupanda na kutunza miti linafanikiwa, pia ili kuhakikisha upandaji miti unakuwa ni endelevu Halmashauri inashirikisha vikundi vya mazingira vilivyopo mjini kutoa hamasa ya upandaji wa miti na kuhifadhi mazingira,”amesema Elizabeth.

/* */