RC Malima apiga marufuku matumizi ya daraja ‘dogo’ la JPM

MKUU wa Mkoa wa Mwanza (RC), Adam Malima, amezuia magari kupita katika daraja la muda linalotumiwa na mkandarasi kupitishia vifaa vya kujengea daraja la John Pombe Magufuli, lililopo Kigongo-Busisi, akisema utaratibu huo umekuwa ukiwachelewesha mafundi kutekeleza ujenzi wa daraja hilo.

Kuanzia sasa magari yatakayoruhusiwa kupita ni ya wagonjwa na Polisi tu, amesema RC baada ya Mkandarasi Mkuu wa Mradi, Mhandisi Jie Hao, kupeleka malalamiko ofisini kwake leo.

“Vinginevyo, mwenye dharula nyingine aombe kibali kutoka kwa Katibu Tawala wa Mkoa, lakini bado tutawalisiliana na wajenzi watuambie ni muda gani wanaweza kuruhusu gari kupita.

“Vinginevyo sisi wote, nikiwemo mimi mwenyewe tuendelee kutumia usafiri wa vivuko, ” amesema.

Kwa mujibu wa Malima, Mkandarasi amelalamika kwamba magari yanayopita ni zaidi ya 100 kwa siku, hali inayosimamisha shughuli za ujenzi mara kwa mara.

Taarifa nyigine aliyopokea kutoka kwa Hao, ni kwamba kutokana na vifaa vingi kutoka nje ya nchi, badala ya ujenzi kukamilika mwezi Februari 2024, litakamilika mwishoni mwa mwaka 2024.

Wakati huohuo, RC amewaonya wanaojihusisha na wizi wa vifaa vya ujenzi, akasema vyombo vya sheria vitashughulika kuanzia na anayefanya mpango, anayebeba, anayenunua na mtumiaji wa mwisho wa vifaa hivyo.

“Atakayekamatwa atakua mfano kwa wengine na uchunguzi wa awali umeshaonesha walipo wanunuzi wa vifaa hivyo,” ameonya.

Habari Zifananazo

Back to top button