RC Manyara atoa siku tano vijana kulipwa milioni 27/-

MKUU wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amemuagiza Mkurugenzi wa Hanang, Francis Namauombo kukilipa kikundi cha vijana deni la Sh milioni 27.5 ndani ya siku tano wanayoidai halmashauri baada ya kufanya kazi kutengeneza madirisha ya shule.

Sendiga ametoa maagizo hayo leo baada ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM ), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda kutoa maelekezo ya chama kwa Mkuu wa Mkoa kuhakikisha kikundi cha Vijana wanaodai fedha zao kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Hanang. Francis Namaumbo zinalipwa.

“Vijana wana haki kwa namna nilivyosikiliza vyema malalamiko na majibu ya mkurugenzi wetu hivyo naomba nikuhakikishie ndugu mwenezi Makonda kama serikali ilifanya ubovu wa kusainj hati mbovu na ubovu huo huo wautumie kuwalipa pesa zao vijana hawa na namuagiza hapa mkurugenzi huyu wa Hanang kuhakikisha ndani ya siku tano hadi kufikia Januari 30 pesa hizo zote Sh milioni 27.5 ziwe zimelipwa kwa vijana hao.” alisema Sendiga.

Awali akizungumza kwa niaba ya vijana hao, Timothy Kalori huyo alimueleza Makonda wakati aliposimama kuwasalimia Wananchi wa mji mdogo wa Katesh akiwa njiani kuelekea mkoani Singida kuwa walifanya kazi ya kutengeneza madirisha ya shule yenye thamani ya Sh milioni 27.5 na mhandisi wa wilaya alishawapatia hati ya kuonesha kumalizika kwa kazi hiyo tangu Septemba, 2023 na bado hawakulipwa.

Alieleza kuwa baada ya kusikikia ujio wa Makonda Halmashauri hiyo waliwaita na kuwapelekwa kwenye shule hiyo na kuwaambia kuwa hakuna ubora wa kazi aliyoifanya na kumtaka kijana huyo ailipe halmashauri hiyo Sh milioni 13.5 hali iliyomsababisha kutokukubaliana na uamuzi huo.

Baada kusikiliza pande zote mbili, Makonda alibaini makosa ndani ya Ofisi ya Mkurugenzi na kumtaka Mkuu wa Mkoa wa Manyara kwa mamlaka aliyonayo kutoa neno na ndipo akaagiza ndani ya siku tano mkandarasi huyo awe ameshalipwa fedha hizo.

“Tunawezaje kuwajengea uchumi wa vijana wa nchi yetu kama iwapo hata kazi wanazofanya kwenye Serikali yetu hamuwalipi? Rais Samia anawapenda vijana na kuwaamini, kufanya hivi ni kumkosea na kuwanyima haki bijana wetu,” alisema Makonda.

Makonda alisema wameamua wao kwenye chama kuipeleka serikali maabara, waipime kidogo ili waone wapi kuna shida.

“Chama hiki hakipaswi kushindwa na hakuna sababu ya kushindwa kwasababu serikali ina bajeti na watendaji mpaka serikali za mitaa, tunataka chama chetu kiwe cha ukweli kushughulikie kero za wananchi kwasababu heshima ya Chama Cha Mapinduzi ni kutatua changamoto za wananchi,” alisema.

Alibainisha kuwa wao hawapendwi,hawaeshimiki kwasababu ya nguo zao za kijani na njano bali wanapenda na kuheshimika kwasababu ya wananchi wamewapatia kura ndipo wakafanikiwa kujenga serikali ambayo inawafanyia kazi wananchi.

Mbali na hayo, Makonda alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na wananchi wote kwa ujumla ikiwemo Viongozi wa Dini, Kimila na Taasisi mbalimbali kufika Hanang kuungana na wananchi wa eneo hilo kuwapa misaada mbalimbali kutokana na maafa waliyoyapata siku za hivi karibuni.

“Tunamshukuru sana Rais wetu kuonyesha uongozi hodari na mahiri kwa kuacha kilakitu kuja kuungana nasi kwa vitendo, tunamshukuru kwa jitihada alizozichukua kuhakikisha nduguzetu 139 ambao walikuwa hawana makazi kabisa, kuendelea kuwahudumia ambapo mpaka leo wako chini ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan,”

“Tunawashukuru watanzania wote walioshikama, tuliwaona viongozi wa Dini, kimila, Taasisi mbalimbali wamefika na wakawashika mkono na ndiyo maana Taifa letu limepata heshima kubwa ya kupambana na majanga, kuyatatua na kurekebisha miundombinu,” Alisema.

Sambamba na hayo pia Makonda alipokuwa akipokelewa mkoani Singida alimuagiza mkurugenzi wote nchi kuacha kuwatumia maofisa kilimo kama wakusanyaji wa mapato katika Halmashauri zao badala ya kuwafuata wakulima mashambani kutoa elimu ya kilimo.

Habari Zifananazo

Back to top button