RC Mara aonya wanaokwamisha upanuzi wa mgodi

Mkuu wa Mkoa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee, akizungumza leo wilayani Tarime. (Picha na Editha Majura).

MKUU wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee, ameagiza yeyote anayekwamisha maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan, katika utekelezaji wa upanuzi wa uwekezaji kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara abadilike haraka.

Alisema hayo baada ya kuelezwa na Meneja Mkuu wa Mgodi huo, Apolinary Lyambiko kuwa baadhi ya wananchi wamekataa kupokea fidia za maeneo na mali zao zilizo kwenye Kijiji cha  Komarera, kwamba mpaka sasa kuna Sh Bilioni 2.5 zilizobakia mgodini.

“Watu wamesusa, baadhi wanalalamika kwamba malipo ni madogo, wengine wanataka tathmini ifanyike tena hatua ambayo ni vigumu kutekelezwa,” alisema Lyambiko.

Advertisement

Aliomba iundwe kamati maalumu itakayoshirikisha wajumbe kutoka mkoani, wilayani, mgodini na wawakilishi wa wananchi, ili majadiliano yatakayowezesha kutatua changamoto hiyo yafanyike.

Naye mthamini kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rashid Mageta, alisema baada ya kampuni binafsi ya WhiteNights kushindwa kufanya uthamini Juni 2020, Wizara hiyo ilifanya utambuzi wa watu na mali zao, kabla ya tathmini waliyoifanya kuanzia Juni 2021.

Alisema licha ya wananchi kukiuka zuio la serikali kwa kuendelea kuotesha mimea na kujenga nyumba kwenye maeneo yao ili walipwe fidia kubwa, tathmini hiyo ilikamilishwa Desemba 2021 na kubaini watu 6,847 walistahili kulipwa huku tegesha wakiwa 5,276.

Rais Samia akiwa ziarani mkoani Mara, Februali Mwaka huu, alikemea tabia ya tegesha na kuagiza wanaostahili walipwe haraka, wasiostahili waachwe.

Awali Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angelina Mabula aliagiza yeyote ambaye hakuwa kwenye eneo hilo, wakati picha za utambuzi zikichukuliwa,  asilipwe.

Naye RC Mzee alisema ikiwa kiongozi mkuu wa nchi ameishatoa maagizo, kinachotakiwa ni utekelezaji hivyo yeyote anayekwamisha ajitathmini na kuchukua hatua haraka.

Kikao hicho kilichojumuisha wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama za mkoa huo,  Wilaya ya Tarime na viongozi wa kada tofauti wa mgodi huo.