RC Mbeya awatolea uvivu Ihefu

MKUU wa mkoa wa Mbeya Juma Homera, ameitaka timu ya soka ya Ihefu kujitathmini kwa wachezaji kuacha kucheza kwa kutumia ukubwa wa majina yao na badala yake wakiwa uwanjani wafanye kile kinachotarajiwa na mashabiki ambacho ni matokeo mazuri.

Pia amelitaka benchi la ufundi la timu kujitafakari juu ya matokeo mabovu tangu kuanza kwa ligi ambapo imepoteza mechi zote tatu za mwanzo.

Homera aliyasema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita alipotembelea maskani ya timu hiyo iliyopo Mbarali mkoani hapa.

Alisema uongozi wa mkoa hautasita kumshawishi mmiliki wa timu hiyo kuvunja benchi la ufundi kama timu itaendelea kupata matokeo mabovu.

Alisema, Ihefu ina kikosi kizuri lakini kinachoonekana ni wachezaji kutumia majina yao makubwa badala ya kuwekeza kwenye nia na bidii ya kuwezesha kupata matokeo mazuri.

“Usichezee mpira jina lako, cheza kiwango ulicho nacho na kuzidisha mazoezi. Ninachokiona ninyi mna timu nzuri sana lakini hamjajua nyakati gani za kukaza..nyakati gani ucheze mpira wa kawaida, Ukibaki kusema mimi nina Chirwa (Obrey) Tshishimbi (Papy)..sijui Juma Nyoso kama hakuna mipango si sahihi,”alisisitiza Homera.

“Hii ligi si ndogo,benchi la ufundi mjitathmini kama mtaendelea kupoteza mechi sisi tutamshauri mkurugenzi  avunje benchi la ufundi. hapa inatumika fedha kulipa mishahara, bonasi hakuna mtu anacheza mpira bure hapa wote mnalipwa mishahara, sasa mtu anajitoa analipa mishahara halafu nyinyi hampati matokeo.”

Homera pia aliwasihi wachezaji kutoathiriwa kisaikolojia na matokeo mabovu waliyoyapata.

“Ukiathirika kisaikolojia mtaendelea kupigwa tu.. mkajitengeneza vizuri kisaikolojia mtafanya vizuri, mechi kama ile ya Mtibwa mie nimeiangalia mwanzo mpaka mwisho … ni presha ambayo wale Mtibwa waliiongeza  mabeki huku chini wakajichanganya..saikolojia ya mpira ukishaona  kwamba mpinzani wako kasawazisha goli  kaa jiulize, jipangeni muongeze  umakini, lakini sasa ninyi mkapoteana kabisaa.. mkaona sasa yule anacheza vile huyu anacheza hivi.”

Aliwasihi pia wachezaji na benci la ufundi kutambua kuwa muda ni mali hivyo mechi wanazozipoteza kwenye mzunguko wa kwanza watakuja kuzikumbuka kwakuwa zitawapa wakati mgumu kwenye mzunguko wa pili wa ligi.

“Mimi hizi timu nazifahamu.. ukifanya mchezo mechi za awali za mzunguko wa kwanza ujue unajitengenezea mzigo kwenye mzunguko wa pili… na hizi mechi zinazopotea mtakuja kuzikumbuka mbele,” alisisitiza.

 

 

 

 

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button