RC Morogoro atahadharisha utapeli wa viwanja

MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Fatma Mwassa amewatahadharisha wananchi wa mkoa huo kuepuka kuwashirikisha watendaji kata ,vijiji, mitaa na wenyekiti wao katika masuala ya mauziano ya ardhi na viwanja kwani yatakuwa ni batiri na hayatambuliki kisheria .

Mwassa ametoa tahadhari hiyo Novemba 30, 2022 wakati wa mkutano wake wa hadhara na wananchi wa mitaa ya Kiegea “A” na “B” baada ya kupokea taarifa ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro , Ally Machela kuhusu utekelezaji wa mradi wa viwanja ekari 4,500.

Amesema wananchi wa mkoa huo wenye kutaka kuuza viwanja ama ardhi zao wanapaswa kufuata sheria zilizopo kwa kuwatumia wanasheria wa halmashauri za wilaya zao na halmashauri ya Manispaaya Morogoro kwa vile tayari fumu maalumu zimeandaliwa za mikataba ya mauziano kwa mujibu wa sheria .

Advertisement

Pamoja na hayo mkuu wa mkoa amewasifu wananchi wa maeneo hayo kwa kuonesha busara na uvumilivu kubwa wakati wote wa mgogoro huo.

Mwassa amewaomba wananchi hao wavitumie viwanja hivyo kwa hekima na burasa kwani ni mali, na wasiviuze ovyo na wakumbuke kuwagawia watoto wao kwa vile miaka ijao hawatamudu kununua viwanja Morogoro mjini.

“ Nimeambiwa mtu mmoja anaweza kuwa na viwanja zaidi ya kimoja , sasa msiuze hovyo bali wamilikisheni watoto wenu nawagawia hii ni asset msiwaache maskini watoto wenu” alisema Mwassa

Mkuu wa mkoa pia amewaomba wanaume wenye kupata viwanja vingi zaidi wasivitapanye ovyo bali wawakumbuke kuwaandikisha wake zao.

Pamoja na hayo mkuu wa mkoa ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi hao wafuate utaratibu wa kisheria wa kuwa na hati , michoro ya ramani na kupata kibali cha ujenzi wanapokuwa tayari kujenga nyumba zao .

“ Ni marufuku kujenga bila kupata hati ni marufuku kujenga bila kuwa na kibali ch ujenzi , ukijenga bila kibali cha ujenzi madhara yake ni kwamba serikali inaweza kubomoa bila ya kukulipa fidia , kujenga bila vibali si jambo zuri “ amesema Mwassa.

Pamoja na hayo amewashauri kuwa endapo wanahitaji kuuza baadhi ya viwanja vyao ili kupata fedha za kujenga nyumba zao ni vyema wafuate utaratibu wa kisheria kwa kuwatumia wanasheria wa Manispaa kwa vile mikataba imeandaliwa kwa mujibu wa sheria .

“ Musiende kwa mtendaji kata , mtendaji wa mtaa, mtendaji wa kijiji na wala mwenyekiti wa kijiji kwani mauziano yoyote kupitia watu hawa ni batiri na hayatatambulika ,wao hawana mamlaka ya kisheria wanachofanya ni utapeli na usanii “ amesema Mwassa.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *