RC Mtwara aipongeza JWTZ kung’ara kikapu kimataifa

RC Mtwara aipongeza JWTZ kung’ara kikapu kimataifa

MKUU wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas, amepongeza timu ya wanaume ya kikapu ya JWTZ kwa kuwa miongoni mwa timu bora za majeshi duniani kwenye mchezo wa kikapu.

Ametoa pongezi hizo leo wakati akifungua kikao Cha kamati ya Utendaji ya Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA), mkoani Mtwara.

“Niwapongeze kwa dhati timu ya wanaume ya basketball ya JWTZ kwa uwakilishi wa mafanikio katika Michezo ya Majeshi ya Dunia ya Basketball nchini Ujerumani,” amesema.

Advertisement

Timu hiyo imefika hatua ya nusu fainali Kati ya timu bora dunian za majeshi 23 kwa kushika nafasi ya nne na kutoa mchezaji bora wa Mashindano.

Amesema hatua ya timu hiyo ni heshima kubwa kwa Tanzania, huku akisema wanamichezo wengi wa Tanzania ambao wamefanikiwa kuiletea sifa na kuitangaza vyema nchi kupitia michezo wametoka katika vyombo vya ulinzi na usalama.

“Wachezaji kama Filbert Bayi, Juma Ikaanga, Samson Ramadhan , Makoye  Isangura,  Alphonce Simbu , Seleman Kidunda , Baraka Sadiki na wengine ambao wametoka katika vyombo vyetu vya ulinzi wamefanikiwa kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania,” amesema.

Katika hatua nyingine, aliwataka wajumbe wa BAMMATA kutumia uwezo wao na weledi katika uongozi wa michezo kusimamia na kuongoza shughuli za maendeleo ya michezo kwa vyombo vya ulinzi na usalama, bila kuathiri sheria na kanuni za michezo.