RC: Sayansi na Teknolojia kichocheo mapinduzi ya kilimo, viwanda, afya

DAR ES SALAAM: MAENDELEO ya sayansi na teknolojia ndani ya jamii ya watanzania yatakuwa ni kichocheo kikubwa katika mapinduzi ya kilimo, viwanda na afya.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ambaye ni Mlezi wa Chama cha Bioteknolojia Tanzania (BST), Adam Malima amesema hayo alipokuwa akifungua mkutano wa wadau wa bioteknolojia pamoja na mkutano mkuu wa mwaka 2023 wa chama hicho mkoani Dar es Salaam.

Malima amesema taifa haliwezi kubadilika bila kuwa na uelewa wa mabadiliko ya kisayansi yanayofanyika duniani.

Advertisement

“Kwenye maendeleo ya kilimo, ufugaji, uvuvi na mazingira hatutaweza kubadilika bila kuwa na uelewa wa mabadiliko ya kisayansi yanayofanyika duniani.

“Maendeleo ya sayansi yanaendana na fursa, yanaendana na utashi wa kisiasa pia,”amesema.

Ameongeza kuwa jitihada ya kuwa na mchango mkubwa zaidi ya baiteknolojia kwenye masuala ya uchumi na jamii ya Tanzania ni jambo ambalo kama waanzilishi wa BST wamelihimiza kwa muda mrefu tokea mwaka 2016.

“Naamini kwamba serikali ya awamu ya sita ina utashi mkubwa sana wa kisiasa kwenye masuala ya sayansi na kwa maana hiyo ni fursa ya wana sayansi kutumia elimu yao na vipaji vyao kuangalia namna ambavyo wao watakuwa ni wachangiaji wakubwa kwenye maendeleo ya Tanzania tunayokusudia,” amesema.

Ametolea mfano upatikanaji wa samaki ndani ya Ziwa Victoria umepungua katika miaka ya sasa, hivyo ni lazima kuangalia njia ya kufanya ili kurudisha wingi wa samaki.

“Lazima tuwe na matumizi ya ufugaji wa kisasa wa samaki, kwenye mifugo tuna ng’ombe wanachangia maziwa kidogo, wanachangia nyama kidogo tunafanyaje wawe na mchango mkubwa zaidi wa maziwa na nyama ndio mambo ambayo hatutarajii kuyapata isipokuwa kwa utafiti na mchango mkubwa wa baiteknolojia,” amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa BST, Profesa Peter Msolla amesema wataendelea kutumia matokeo ya utafiti na taarifa za kisayansi katika kuhamasisha na kujenga uwezo na uelewa wa vijana juu ya fursa zinazotokana na matumizi salama na endelevu ya bioteknolojia kwenye minyororo ya thamani mbalimbali.

Amesema matumizi ya bioteknolojia ya kisasa duniani yameleta manufaa makubwa kwenye sekta za kilimo, afya, mifugo, viwanda na mazingira.

“Mifano iko mingi lakini niruhusu nitaje michache, uzalishaji wa aina bora za mazao mbalimbali yenye uwezo wa kuzaa kwa wingi na yenye ukinzani dhidi ya visumbufu vya magonjwa na wadudu, utengenezaji wa dawa za kukabiliana na magonjwa sugu kwa mfano insulin kwa ugonjwa wa kisukari, chanjo za VVU/UKIMWI, UVIKO-19 na malaria, na uzalishaji wa mbolea na gesi kutokana na taka za mashambani na viwandani,” amesema.

2 comments

Comments are closed.