MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahya Nawanda ameahidi kusimamia na kuhamasisha wananchi kushiriki kuchangia huduma ya chakula shuleni na kusema hadi kufikia Januari mwakani, shule zote Mkoa wa Simiyu zitakuwa zikitoa huduma ya chakula kwa wanafunzi.
Amesema chakula hicho kitolewe asubuhi na mchana, ili kuwawezesha wanafunzi kuzingatia masomo na kupunguza tabia ya utoro.
Akizungumza na wananchi wa Kata za Isanga, Nhuhu na Buchambi zilizoko Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, wakati wa uzinduzi wa miradi ya kutoa huduma za maji safi na salama inayotekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Wilayani Maswa (MAUWASA), alisema hadi Januari mwakani shule zote za Simiyu zitakuwa zikitoa huduma ya chakula, hivyo kilichobakia ni kuangalia namna ya upatikanaji wa fedha hizo, ambazo aliahidi kushiriki na kuchangia kuanzishwa kwake.
Aliwataka wananchi pia kuunga mkono mpango huo, ili kupunguza changamoto zinazoendelea kutokea za kuwepo na idadi kubwa ya wanafunzi kukwama kuhudhuria masomo, au kufika shuleni kwa kukosa huduma muhimu, kama chakula, ambazo zimekuwa zikitolewa kwa shule nyingi maeneo ya mijini.
Alisema kumekuwa na ongezeko la utoro shuleni, hasa kwa watoto wengi wanaotoka katika mazingira duni na wanaoishi maeneo ya mbali na shule wanazosoma, miongoni mwa vitu vinavyochochea hali hiyo ni kukosekana huduma ya chakula.
“Kama serikali lengo letu ni kuhakikisha watoto wote waliofikia umri wa kwenda shule wanaenda shule na kushiriki muda wote wa masomo shuleni hapo, pamoja na kupatiwa huduma ya chakula, ili kupunguza utoro kwa wanafunzi hao.
“Hivyo tumeamua kama Mkoa wa Simiyu kusimamia hilo na kuhakikisha hakuna tabia ya utoro kwa Mkoa wa Simiyu,” alisema Dk Nawanda.
Pia alizungumzia changamoto zingine zinazosababisha watoto wengi kutoenda au kutohudhuria muda wote wa masomo, ni kutokana na hali ya ukosefu wa huduma za maji safi na salama katika baadhi ya maeneo Mkoa wa Simiyu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge alisema kuwa licha ya kuwepo kwa Bwawa la Zanzui, ambalo ndilo chanzo kikuu cha kutolea huduma za maji kwa Wilaya ya Maswa, bado kulikuwa na changamoto ya kukosekana kwa huduma hiyo kwa baadhi ya maeneo hasa ya vijijini, hivyo kuanzishwa kwa vituo hivyo kutasaidia kumaliza changamoto hiyo kwa wanafunzi.
Naye Meneja wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijini (Ruwasa) Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Mariam Majala, alisema kuwa ujenzi wa miradi hiyo umekamilika kwa asilimia 100.