HALMASHAURI ya Wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu, imetumia kiasi cha Sh milioni 356, katika ujenzi wa mradi wa maji safi na salama utakaowanufaisha Wakazi wanaokadiliwa kufikia 2,427 wa kijiji cha Isengwa, Wilaya ya Meatu, ambao walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo.
Katika ziara aliyofanya wilayani Meatu mwishoni mwa wiki, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahya Nawanda, alisema upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa maeneo hayo, utapunguza adha walizokuwa wakikabiliwa nazo za kutembea umbali mrefu na kutumia maji yanayopatikana katika mito.
Alisema kuwa suala la upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa maeneo yote ya Mkoa wa Simiyu, ni jambo ambalo ni mkakati katika uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na lengo ni kuhakikisha wanafikia asilimia 85 ya wakazi wa mjini na asilimia 75 kwa wakazi wa vijijini wanaoishi Mkoa wa Simiyu.
“Kuanza kutumika kwa mradi huu utapunguza adha ambayo wananchi walikuwa wakiipata, kwa kutumia maji ambayo huwa si salama, ambayo huyapata katika maeneo ya mito na pia huwa hatarishi kwa afya ya wakazi hao kutokana na kutumiwa na wanyama na kuchanganyikana na maji taka kutoka sehemu zingine za eneo hilo,” alisema Dk. Nawanda.
Akizungumza wakati akitoa taarifa mbele ya Mkuu wa Mkoa, kabla ya kuweka jiwe la msingi kwenye mradi huo, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Wilaya ya Meatu, mhandisi George Masawe, alisema kuwa hadi kuanza kutumika kwa mradi huo utakuwa na uwezo wa kuzalisha lita 25,000 za maji kwa siku.
“Mahitaji ya maji Isengwa ni lita 20,675 kwa siku, huku uzalishaji wa chanzo ukiwa lita za ujazo 1,025,000, kwa siku na hivyo kukidhi mahitaji ya maji kwa wananchi wote wanaoishi katika kijiji hicho na kuongeza upatikanaji wa maji wilayani hapo kwa asilimia 0.8 na hivyo kufikia asilimia 68.1,” alisema.
Kwa upande wake Meneja wa RUWASA Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Mariam Majala, amesema ni muhimu chombo cha watumiaji wa maji ngazi ya jamii (CBWSOs), kikafuata bei elekezi, ambazo tayari zimeshatangazwa, huku akisisitiza kuwa bei ya maji kwa wanaotumia nishati ya jua ndoo ni Sh 30, jenereta ndoo ni sh 50 na umeme ndoo sh 40.
Nao baadhi ya wananchi wamesema awali walitembea umbali mrefu kufuati maji, ambapo wakati mwingine hayakuwa safi na salama, hivyo mradi huo umekuwa mkombozi kwao.
“Tunaishukuru Serikali ya Rais Samia kwa kutuletea huduma hii ya maji, kwa kuwa tumekuwa tukitembea umbali mrefu kufuata maji katika mito, ambapo kwa kipindi cha kiangazi hukauka, hivyo kusababisha adha kubwa kwa watumiaji wa maji na wakazi wa eneo hili kwa ujumla,” alisema Pendo Emmanuel mkazi wa eneo hilo.