RC Singida aagiza uchunguzi tuhuma za mauaji

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akizungumza kwenye mkutano wa hadhara (Picha zote na Editha Majura).

VILIO vya wananchi kuuawa hovyo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, mkoani hapa vimefikishwa kwa Mkuu wa Mkoa, Peter Serukamba, ambaye ameagiza vyombo vya dola vikiongozwa na Ofisa wa Usalama wa Taifa wa wilaya hiyo (DSO), kuchunguza na kukomesha matukio hayo.

Prisca Maleta, mkazi wa Manyoni huku akipigiwa makofi na karibu wananchi wote waliohudhuria mkutano wa hadhara wa Serukamba, uliolenga kusikiliza na kutoa ufumbuzi wa kero za wananchi jana, amesema vifo vya watu vimekithiri kiasi cha kila wiki kuokotwa mwili wa mtu aliyeuawa.

“Siyo kwamba wananchi hatufahamu wahalifu, la hasha tatizo ni jeshi la polisi, mfano, mimi nikitoa taarifa kwa polisi kabla mtuhumiwa hajakamatwa tayari anafahamu Prisca ameniripoti moja, mbili, tatu…,” amesema.

Advertisement

Prisca Maleta akieleza kero zake mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Singida.

Maleta amesema hali hiyo inasababisha visasi ambavyo wananchi wanaamini ni moja ya chanzo cha mauaji hayo na amesema baadhi ya askari, anaowafahamu kwa sura na majina, wanamiliki pikipiki ambazo wamewapatia vijana wanaofanya ‘kazi hizo’.

Amesema yupo tayari kumtajia Serukamba askari hao, (siyo kwenye mkutano) endapo atatakiwa kufanya hivyo na kwamba vijana wanaotumia pikipiki za askari hata wanapofanya uhalifu mkubwa na kulalamika polisi, hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi yao.

Hata hivyo amemshukuru Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) hiyo, Ahmed Makelle, kwamba anawapa ushirikiano mkubwa maelezo yaliyoungwa mkono na wananchi wengi kwa kushangilia na kumpigia makofi.

Naye Khalfan Poloto amelalamikia jeshi hilo kitengo cha upelelezi kuwa mtu anapopeleka mashitaka kituoni na kufunguliwa jadala, badala ya kukutanishwa na askari mpelelezi wa kesi yake hupewa namba ya simu na kila ikipigwa muhusika husema yupo nje ya wilaya.

“Mimi nilipeleka kesi ya wizi nikapewa namba ya simu ya mpelelezi nilipompigia akataka nimpe namba ya simu ya mshukiwa, alipigiwa simu akimuita kituoni lakini mshukiwa alipofika hakumkuta ayelimuita,” amesema.

Poloto amesema alipompigia simu mpelelezi huyo, akamwambia alikuwa nje ya Manyoni.

Pia amesema Pikipiki ya rafiki yake iliibwa, kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa mtaa pamoja na balozi walikamata watu watatu wakiwa na pikipiki hiyo na kuwafikisha kituo cha polisi, wakapewa namba ya simu ya mpelelezi wa kesi hiyo.

Amesema aliyepokea simu hiyo alisema alikuwa nje ya Manyoni, watuhumiwa walikaa mahabusu kwa siku tatu bila hatua yoyote kuchukuliwa hali iliyosababisha mlalamikaji kuomba waachiwe.

Kwa mujibu wa Poloto tatizo hilo limekuwa sugu kwenye idara ya upelelezi ya polisi wilayani humo, hali inayowafanya waamini huduma haziwezi kuwa na ubora unaotakiwa kutokana na unyeti wa idara hiyo.

Makere ametakiwa na Serukamba kutoa majibu kwa wananchi, akakiri kukithiri kwa vifo visivyo vya kawaida, lakini amekanusha kuwa chanzo ni visasi.

“Siyo vifo vya kawaida, siyo vya kisasi wala siyo vifo vya kuwania mali, kusema mtu ameuawa kwa sababu ana pesa au mwizi anataka aibe vitu kwake, inatafutwa kata fulani ambayo ina (low profile),” amesema Makere na kuendelea:

Khalfan Poloto akizungumza kwenye mkutano huo.

“Mtu anauawa na kuchukuliwa vitu muhimu aidha nguo za chini za mwanaume huzikuti kwenye maiti zote, lakini nimeanza kuchukua hatua, kuna baadhi ya watu ninao kwa ajili ya mahojiano.”

Amesema ataendelea kufanya hivyo mpaka apate taarifa sahihi, zitakazowezesha kukomesha hali hiyo na kwamba hata kabla ya mauaji hayo, makaburi yalikuwa yakifukuliwa ambapo uchunguzi ulibaini kiini kilikuwa imani za ushirikina, vilitakiwa vitu vinavyohusiana na maiti.

Serukamba amemtaka RSO kuunda timu ikishirikisha vyombo vya dola wilayani humo, ichunguze na kubaini washirikina, wauaji na wanaofukua makaburi ili wakomeshwe.

Amesema haiwezekani serikali ipo halafu watu wauawe hovyo na kwamba ifikapo Ijumaa, Januari 27 Mwaka huu apelekewe taarifa kamili ya uchunguzi huo, askari wanaotuhumiwa kuvujisha siri za watoa taarifa za uhalifu na wapelelezi wanaowasiliana na walalamikaji kwa simu wakiwa nje ya wilaya ili hatua stahiki zichukuliwe.

 

OCD  Ahmed Makelle akizungumza kwenye mkutano huo.
Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *