RC Tanga aitaka CWT kuheshimu sheria

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba amekitaka Chama cha Walimu (CWT) kuheshimu utawala wa sheria uliopo kwa kutochagua wagombea ambao nafasi zao zimewekewa zuio la kimahakama.
Aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu maalumu wa uchaguzi wa chama hicho unaofanyika mkoani Tanga.
Alisema ni lazima mhimili huo wa dola uweze kuheshimiwa maamuzi yake.
Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma jana imepokea ombi la zuio la kimahakama linalotaka mkutano Mkuu wa CWT usifanye uchaguzi kwa nafasi za Katibu Mkuu na Mwekahazina.
Aidha, Mkuu wa Mkoa aliwaelekeza kuendelea na uchaguzi katika nafasi za Makamu wa Rais, Katibu Msaidizi pamoja na mjumbe wa kitengo cha wanawake.
“Niwaase wakati wa uchaguzi mchague viongozi ambao wataendelea kuleta heshima ndani ya chama na nje, na sio ambao watawagawa kwa ukabila, udini pamoja na makundi lakini kubwa ni kumweka kiongozi kwa njia za rushwa,” aliwaasa Kindamba.
Aidha, alisema chama hicho kinaongoza kwa wingi wa wanachama hapa nchini hivyo ni matumaini yake watakwenda kufanya uchaguzi ambao utajali maslahi sio tuu ya kada hiyo ya walimu bali nchi nzima kwa ujumla.
Kwa upande wake, Rais mstaafu wa chama hicho, Gracias Mkoba alisema ni muhimu wajumbe hao kuzingatia kuchagua kiongozi ambaye atakwenda kubeba maslahi na dhana nzima ya msingi wa uwepo wa vyama vya wafanyakazi.
“Niwaombe msiruhusu rushwa iingie kwenye chama chetu kwani italeta athari kubwa mbeleni, ni lazima tuendelee kulinda hadhi na sifa ya chama chetu,” alisema Mkoba.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa CWT, Josephat Maganga aliishukuru serikali kwa kusikia kilio chao cha kupandishwa madaraja pamoja na vyeo ikiwemo malipo ya stahiki zao mbalimbali.