MKUU wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba amesema kuwa Tanga kwa sasa sio kichaka cha bidhaa za magendo na dawa za kulevya.
–
Kauli hiyo ameitoa leo wakati wa uzinduzi wa boti maalum ya kudhibiti uingizwaji wa bidhaa za magendo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Tanga.
–
Amesema kuwa mkoa huo umeshapata suluhisho, hivyo watazidi kuwa wakali katika kudhibiti magendo ili mapato yasipotee, lakini pia kudhibiti masuala ya uingizaji wa dawa za kulevya ‘unga’.
–
Hata hivyo ameitaka TRA mkoani hapa kutumia njia rafiki katika ukusanyaji wa mapato, ikiwemo kufanya maridhiano, ili wafanyabiashara waweze kulipa kodi kwa hiari yao.
–
Naibu Kamishna wa Forodha na Ushauri Geofrey Katundu, amesema kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Desemba mwaka jana, bidhaa za magendo zenye thamani ya Sh Bil 11.05 zilikamatwa, ambapo baada ya tozo na adhabu zililipwa Sh Bil 13.1.
–
“Kwa mkoa wa Tanga pekee bidhaa za magendo zenye thamani ya Sh Mil 675 zilikamatwa, ambapo baada ya tozo na adhabu zililipiwa Sh Mil 799,”amesema Katundu.
–
Amesema kuwa ununuzi wa boti hiyo yenye thamani ya Sh Mil 529, itakwenda kuwa mkombozi katika jitihada za kudhibiti vitendo vya ukwepaji wa kodi kupitia bidhaa za magendo.
–