RC Tanga aonya uharibifu wa mazingira

RC Tanga aonya uharibifu wa mazingira

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba amewataka viongozi katika mkoa huo, wakiwemo wakuu wa wilaya  kutowaonea haya wanaoharibu mazingira, badala yake kuwachukulia hatua kali za kisheria.

Kindamba ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti Mkoa wa Tanga mwaka 2023 iliyofanyika eneo la Shule ya Msingi Usagara jijini Tanga, yenye lengo la kutoa hamasa kwa wananchi kupanda miti maeneo yao.

” Nawaomba wakuu wa wilaya mkalisimamie hilo, hawawezi watu wakawa wanakata miti na kuharibu vyanzo vya maji halafu tunacheka nao, ukicheka na nyani utavuna mabua na sisi Mkoa wa Tanga hatutotaka kuvua mabua,” amesema Kindamba.

Advertisement

Amesema maelekezo ya viongozi, akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan yapo wazi katika kutunza mazingira sambamba na vyanzo vya maji, hivyo maelekezo hayo yasimamiwe kwa ukamilifu na kwa wakati.

Kwa upande wake katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Pili Mnyema amesema kuwa katika kufikia lengo la upandaji miti milioni 1.5, tayari wameshapanda zaidi ya miti 60,000 katika kipindi cha hivi karibu mara mvua zilivyoanza kunyesha.

“Ni imani yangu mpaka ifikapo mwishoni mwa mwaka huu tutakuwa tumevuka lengo ambalo limewekwa na serikali, hivyo  viongozi wote katika mkoa huo tunawajibu wa  kusimamia vyema kampeni hiyo ya upandaji miti, kuhakikisha inafanikiwa kwa asilimia 100,”amesema Mnyema.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *