MKUU wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba amewataka watumishi mkoani humo kuchapakazi kama ambavyo malengo ya utumishi wao yanavyotaka badala ya kutumia muda mwingi kuomba uhamisho .
Rai hiyo ameitoa wakati akiongea na watumishi wa Halmashauri ya Bumbuli iliyopo wilayani Lushoto amewataka kufanyakazi kwa weledi na kuzitumia changamoto katika eneo hilo kama fursa ya kujiletea maendeleo.
Amesema kuwa amekuwa akipokea barua nyingi za watumishi hao kuomba uhamisho kwa kigezo Cha kuumwa na mazingira magumu ya kazi.
“Niwaambie tuu ukishakuwa mtumishi wa umma wewe unawajibu wa kufanyakazi mahali popote katika mazingira yoyote hivyo niwaombe timizeni wajibu wenu wa kuwatumia wanabumbuli badala ya kuomba uhamisho tuu”amesema RC KIndamba.
Aidha amewataka Watumishi hao kuzingatia miiko na maadili katika ufanyajikazi wao hususani katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye ufanisi na kwa wakati.
Hata hivyo Mkurungenzi Mtendaji wa Halimashauri hiyo George Haule amesema kuwa wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa watumishi hususani katika kada ya elimu na afya.