RC: Wanawake tumieni ‘kicheni pati’ kukuza uchumi

MKUU wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amewataka wanawake watumie ‘kicheni pati’ kupeana elimu ya kukuza na kulinda uchumi wa familia na si ndoa pekee.

Mtaka alitoa mwito huo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kimkoa yaliyofanyika Shule ya Msingi Itutunduma wilayani Njombe.

Alisema kicheni pati pia zitumike kupeana elimu ya kulinda uchumi wa familia zao badala ya kulinda ndoa zao ama kupendwa na waume zao pekee.

Mtaka alisema kwa kuwa wanawake wanakosa elimu ya kukuza na kulinda uchumi wa familia zao, imesababisha migogoro ya mirathi wanapofiwa na waume zao.

Alisema ni lazima wanawake kumiliki uchumi kwa kuhakikisha wanawasomesha watoto wao pasipo kujali jinsia zao.

Naye Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Pindi Chana aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo aliitaka jamii hasa wanawake kusimamia maadili bora ya watoto wao ili kuepukana na vitendo vya ukatili ambavyo vinarudisha nyuma maendeleo.

Wanawake akiwemo Theresia Mbundala na Veronica Malifimbo walisema licha ya kujikwamua kiuchumi wataendelea kuheshimu misingi ya ndoa zao hasa waume zao.

Habari Zifananazo

Back to top button