RC Waziri aeleza mikakati kukabili udumavu

RC Waziri aeleza mikakati kukabili udumavu

MKOA wa Songwe umejipanga kupambana kutatua udumavu na uzito pungufu kwa watoto chini ya miaka mitano, licha ya  kuwa miongoni mwa mikoa inayofanya vizuri katika uzalishaji wa mazao ya chakula.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Waziri Kindamba akizungumza kwenye jukwaa la kujadili sera, changamoto  fursa za watoto kwenye sekta ya afya na elimu, alisema mpaka hivi sasa Mkoa wa Songwe takwimu zinaonesha kuwa udumavu ni asilimia 43 na uzito pungufu ni asilimia 17.

Alisema kiwango hicho ni kikubwa ukilinganisha na wastani wa kitaifa wa udumavu ambapo ni asilimia 32, huku Songwe ikiwa juu kwa asilimia 11 zaidi ya wastani wa udumavu kitaifa.

Advertisement

Alisema miongoni mwa mikakati ya mkoa ni pamoja na kuandaa jukwaa hilo ambalo limeshirikisha sekta za afya na elimu huku wadau mbalimbali na mashirika kutoka ndani na nje ya Tanzania yakishiriki pia.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dk Nyembea Hamad alisema miongoni mwa sababu za kukithiri kwa changamoto za kiafya na kielimu kwa baadhi ya mikoa hasa Songwe ni mgawanyo wa rasilimali fedha kutowiana na hali halisi katika baadhi ya mikoa hivyo kushindwa kutatua changamoto nyingi.

“Pamoja na Songwe kuwa na changamoto kubwa ya miundombinu katika upande wa elimu na afya na waathirika wengi kuwa ni watoto wadogo hasa chini ya miaka mitano, halmashauri za mkoa zimekuwa zikipata mgao kidogo tofauti na baadhi ya mikoa ambayo halmashauri zake zinakusanya mapato ya ndani kwa kiasi kikubwa na kupata kiasi kikubwa cha rasilimali fedha,” alisema.

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Bajeti ya Serikali Mikoa na Halmashauri, Andambike Mololo alisema awali Mkoa wa Songwe ulikuwa unapata mgawo kidogo kutokana na kuwa mkoa mpya wenye halmashauri nyingi mpya ambazo hazikuwa na miundombinu mingi ya kutolea huduma.

Alisema kutokana na mahitaji makubwa ya Songwe kuhusu kuboreshewa huduma katika sekta za afya na elimu watalifanyia kazi haraka na kuleta mabadiliko makubwa kutokana na uhitaji uliopo.

“Serikali inakwenda kufanya mabadiliko makubwa ili kusaidia mkoa uweze kupata mgao mkubwa kulingana na mahitaji, tutapunguza kiwango kwa halmashauri zote zenye uwezo mkubwa wa kukusanya mapato ya ndani,” alisema.