REA, EU wasaini umeme vijijini maeneo 426

WAKALA ya Nishati Vijijini (REA) na Umoja wa Nchi za Ulaya (EU), wamesaini mkataba na wakandarasi 59 kutekeleza mradi wa kuunganisha umeme vijijini katika maeneo 426 wenye thamani ya Sh bilioni 37.

EU ni mmoja wa wafadhili wanaoiunga mkono kifedha serikali kusaidia miradi ya kuunganisha umeme vijijini na mpaka sasa imeshatoa takribani Sh bilioni 169.6.

Akizungumza katika utiaji saini mikataba ya utekelezaji wa miradi hiyo Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Hassan Saidy alisema wakandarasi hao watatekeleza mradi wa kupeleka umeme vijijini katika hospitali sita, vituo vya afya 57 na miradi ya maji 363.

Saidy alisema EU walianza kuunga mkono miradi ya umeme tangu mwaka 2017 kwa kutoa Euro milioni 50 sawa na Sh bilioni 120 kupeleka umeme vijijini.

Alieleza kuwa mwaka 2020, EU iliongeza kwenye mkataba wao wa awali Euro milioni 15 sawa na Sh bilioni 37 kutekeleza miradi hiyo 426 iliyolenga maeneo ya afya na maji.

Aidha, alisema EU ilitoa pia Euro milioni 6.5 sawa na Sh bilioni 14.3 kujenga Kituo cha Kupoozea Umeme Ifakara na kujenga njia ya umeme yenye urefu wa kilometa 98.

“Kwa ujumla EU imechangia katika miradi ya kuunganishia umeme wananchi takribani Euro milioni 71.5 sawa na shilingi bilioni 169.6. Fedha hizi ni sehemu ya michango ya wafadhili wengine zitakazotumika pia kumalizia vjijini 3,448 vilivyobakia kuunganishiwa umeme kati ya vijiji 12,345 vilivyopo nchini,” alisema Saidy.

Alieleza kuwa vijiji hivyo 3,448 vilivyobakia utekelezaji wake unafanyika katika awamu ya tatu; sehemu ya pili kwa ufadhili wa mashirika mengi ikiwamo EU, Benki ya Dunia na Serikali ya Sweden.

Aliwataka wakandarasi hao kuzingatia mikataba yao na kutowaangusha wakandarasi wengine wazawa kwa kutekeleza ipasavyo miradi hiyo na kuikamilisha kwa wakati bila visingizio.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya REA, Styden Rwebangira alisema lengo la miradi hiyo ni kuhakikisha maji tiririka yanapatikana na magonjwa ambukizi yanadhibiwa.

Alisema tangu Tanzania ikumbwe na tatizo la Covid-19, njia mojawapo ya kupambana ilikuwa ni kunawa kwa maji tiririka, lakini pia kwa sasa mamlaka za maji zinapambana kupeleka maji maeneo mbalimbali nchini, lakini haiwezekani kupeleka maji bila umeme.

Aidha, alisema kuna chanjo zinazotolewa ikiwamo ya Covid-19 na magonjwa mengine na changamoto katika vituo vinavyojengwa ambavyo ili vikamilike lazima viwe na umeme na ndio maana EU iliamua umeme upelekwe kwenye vituo vya afya, hospitali na miradi ya maji.

Meneja Miradi katika EU, Francis Songera alisema mradi huo kwa ujumla una thamani ya Sh bilioni 37 na kwamba EU kazi yake itakuwa ni kutoa fedha na REA itasimamia utekelezaji wa miradi hiyo.

 

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x