MBUNGE wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde, amewataka wataalamu wa ardhi wa jiji la Dodoma kurekebisha kasoro zilijitokeza katika zoezi la upimaji ardhi ili kupunguza migogoro ya ardhi isiyo ya lazima.
Mavunde ameyasema hayo katika mkutano wake wa kusikiliza kero za wananchi uliofanyika katika kata ya Ntyuka.
“Nimesikiliza kero zenu ambapo kwa zaidi ya asilimia 80 zimeelekezwa kwenye ardhi na haswa zoezi la upimaji.”Amesema na kuongeza
“Hapa kulikuwa na kampuni binafsi ambayo ndiyo ilikuwa inashughulikia suala la upimaji ardhi,zipo kasoro zimejitokeza hivyo ninawataka wataalamu wa jiji kuhakikisha mnarekebisha kasoro hizo ili kupunguza migogoro ya ardhi isiyo ya lazima.
Amesema, timu ya wataalamu wa ardhi wataweka ili kutatua changamoto hizo kwa wananchi na hii itakuwa ni fursa ya kipekee kushughulikia migogoro yote iliyopo.
“Tunaishukuru pia serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuanza kwa ujenzi wa barabara ya Ntyuka-Mvumi kwa kiwango cha lami,barabara hii itarahisisha sana upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi.”Amesema
Naye Mwenyekiti wa CCM wilaya Dodoma Mjini Charles Mamba amewataka viongozi wote kuhakikisha wanasimamia na kutatua kero za wananchi kama ilani ya uchaguzi inavyoelekeza.
.