Repoa yataka hatua kali ukatili kijinsia
TAASISI ya Utafiti na Kupunguza Umasikini Tanzania (REPOA), imeshauri Jeshi la Polisi kuchukua hatua kali dhidi ya ukatili wa kijinsia ili wanawake wawe na uhuru zaidi wa kufanya shughuli zao bila hofu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Dk Donald Mmari alitoa ushauri huo wakati wa kutoa matokeo ya utafiti yaliyopatikana katika masuala ya usawa wa kijinsia na ukatili wa kijinsia.
Alisema jambo hilo linapaswa kupewa kipaumbele japo matukio ya namna hiyo yanaonekana kupungua lakini yanapojitokeza yana athari kubwa.
“Sisi kama watafiti tunashirikisha taasisi mbalimbali za umma kuona matokeo hayo na jinsi Watanzania wanasema. Lakini tunaangalia na takwimu nyingine zinazotokana na taasisi nyingine ikiwemo Taasisi ya Taifa ya Takwimu kuona maeneo ambayo tunadhani yanapaswa kupewa kipaumbele pamoja na kusikiliza maoni ya wananchi,” alisema.
Mtafiti Mwandamizi kutoka Repoa, Dk Jane Papalika alieleza Tanzania ilivyopiga hatua katika masuala hayo ya usawa wa kijinsia tofauti na miaka ya 1980 na 1990 ambapo kulikuwa na changamoto nyingi zilizohusu elimu kwa mwanamke na umiliki wa ardhi.
Alishauri serikali ifanye jitihada zaidi za kupunguza ukatili wa kijinsia hususani sehemu za vijijini kwa kufanya kampeni kwa kushirikiana na wadau wengine.
Wakili kutoka Mtandao wa Utetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, Nuru Maro alisema zitumike tafiti zinazofanywa na wadau kama Repoa kama nyenzo ya kuleta mabadiliko panapohitajika.
Alishauri serikali kuharakisha mchakato wa kumalizia sheria ya ukatili wa kijinsia unaoendelea kufanyiwa kazi ili kuweka ulinzi wa kisheria na kisera kwa sababu bila sheria madhubuti vitendo hivyo vitaendelea.