Repoa yazungumzia changamoto taasisi za kimtandao

TAASISI ya Utafiti na Kupunguza Umaskini Tanzania (Repoa), imebaini kuwa taasisi  za kimtandao zimekuwa na changamoto ya mawasiliano baina yao kutokana na upya wa sekta hiyo.

Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo wa Repoa, Lucas Katera amesema hayo yamebainika katika utafiti iliyoufanya kuhusu uchumi wa kidijitali wakati wa warsha iliyowakutanisha wadau wanaofanya kazi katika eneo la kidijitali kwa ajili ya kuangalia matokeo, mapendekezo na mikakati ya kuboresha eneo hilo hapa nchi.

Amesema wamebaini kuwa changamoto hiyo imejitokeza kutokana na upya wa sekta hiyo na kutokuelewa jinsi ya kuiendesha.

“Wachache wameingia katika sekta hii, lakini walivyoingia kule hawajawa na uelewa wa kinachoendelea kule, lakini pia kumekuwa na changamoto kati ya mitandao na watunga sera,” amesema.

Amesema kutokana na upya wake bado kujua mikataba ya wafanyakazi wake iwe ya namna gani na malipo yaweje, ndio maana inaonekana ni changamoto.

“Repoa imejiingiza kufanya utafiti huu kwa sababu ni kitu kipya kwa Tanzania namna gani nchi iingie, namna gani kuangalia mikataba mbalimbali ya wale ambao watakuwa wanafanya kazi katika sekta hii na pia kuangalia kwamba namna gani hii sekta ikawa na mawasiliano ya karibu na sekta nyingine ili kuwa na maendeleo ambayo ni shirikishi,” amesema.

Naye Mtafiti Mwandamizi kutoka Repoa, Jamal Msami amesema uchumi wa kidijitali ni mwakisi wa mwenendo wa dunia kwa ujumla na kwamba  uchumi huo una jumla wa dola za kimarekani trilioni 105 ambacho ni kiwango kikubwa.

Amesema katika uchumi huo wa kidijitali fursa ni nyingi kwa kuwa una vikwazo vidogo vya kuingia na kutoka.

“Vikwazo vidogo namaanisha kwamba hauhitaji kuwa na vyeti vya kutosha sana, hauhitaji kuwa na uzoefu wa miaka 100 na kuendelea kama baadhi ya waajiri wanataka, lakini pia tunazungumzia jitihada zako wewe kama unataka kuingia kushiriki katika huu uchumi ndio zitakuwezesha uweze kufanikiwa.

“Unaweza kusema pia ni uchumi wa kiganjani kwa sababu mageuzi na ubunifu uliotokea katika miaka ya karibuni umesababisha maisha kuwa kiganjani.

 

“Leo hii naweza kukaa hapa nikajua mvua itanyesha eneo gani kwa kiwango gani, hali kadhalika kujua bei ya mazao na bidhaa mbalimbali katika maeneo mbalimbali. Pia naweza kufanya biashara na watu walioko katika pembe zote nne za dunia,” amesema.

Amesema hivi sasa kuna watu wanaotoa huduma za usafirishaji, ufundi,  huduma za kitaalam nyingine kama bima, afya na nyingineo kwa kutumia mitandao ya kidijitali.

Naye Ofisa Leseni kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), Romano Chile amesema utafiti huo uliofanywa una faida katika jamii kwa kuwa umekusanyisha wadau tofauti kujadili jinsi ya kuboresha masuala ya taksi mtandao.

“ Sisi kama serikali tumekuja kutoa mchango wa jinsi tunavyofanya kazi suala hili la taksi mtandao katika suala la sheria na taratibu mbalimbali zilizowekwa,” amesema.

Kwa upande wake Meneja Mfuko wa Bima mkoa wa Kinondoni, Innocent Mauki alisema jukumu lao ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya bora kwa watumishi wa sekta rasmi na mwananchi mmoja mmoja.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button