Ridhiwan Kikwete ajitosa mgogoro Chasimba

NAIBU Waziri wa Ardhi, Ridhiwan Kikwete ameahidi kushughulikia tatizo la mgogoro wa ardhi kwenye eneo la Chasimba, Bunju wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na HabariLeo, Ridhiwan amesema tayari amekutana na Mbunge wa Kawe, Joseph Gwajima na kuzungumzia kwa undani mgogoro huo ambao umeibuka upya kwa wakazi wa maeneo hayo kugoma kulipa tozo ya skwea mita na badala yake wanataka kulipa tozo ya Primer kama walivyokubaliana katika kikao cha March 14, 2021 chini ya aliyekuwa Waziri wa Ardhi wa wakati huo Wiliam Lukuvi.

“Nimekutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Joseph Gwajima kujadili mvutano pale Chasimba, nimemuahidi kufuatilia na kutatua changamoto zilizopo.” Amesema

Kauli ya Ridhiwan imekuja baada ya wananchi wa Chasimba kuandamana mwishoni mwa wiki wakimuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati madai yao ambayo wanadai kukiukwa kwani katika makubaliano yao na Waziri wa Ardhi wa wakati huo na watendaji wa Manispaa ya Kinondoni walitakiwa kupima ardhi na kulipa tozo ya premier lakini kwa sasa wanadai kutakiwa kulipa tozo ya Skwea mita ambayo ni shilingi shilingi  6,416.

Salma Mohamed mkazi wa  Chasimba amesema “Lukuvi alikuja akasema nimetumwa na Rais (John Magufuli) nyinyi sio wavamizi mtakaa hapa na mtalipa tozo ya ardhi, wananchi wa Chasimba, Cha Tembo na Cha Chui na alimaliza mgogoro ule.”

Naibu Waziri wa Ardhi, Ridhiwan Kikwete akiteta na Mbunge wa Kawe, Josephat Gwajima

Kwa upande wa Haruni Habibu, mkazi wa Basihaya anasema  “Kiwastani Cha Simba hatuna mgogoro wowote, tulisubiri ahadi zetu tulipe premium ya asilimia 1, viwanja vilishapimwa  chini ya Lukuvi tunachosubiri sasa ni hati zetu tu.”Amesema na kuongeza

“Mgorogoro huo umekuwa ukichukua sura tofauti tofauti kila mara kufuatiwa na mabadiliko ya uongozi wa kinchi hususani mabadiliko ya mawaziri, makubaliano yatakayofikiwa na Waziri wa kipindi fulani yanaweza kubadilishwa anapoingia Waziri mwingine.”Amesema

Mwaka 2015 aliyekuwa Waziri wa Ardhi, William Lukuvi aliingilia mgogoro huo wa kiwanja chenye ukubwa wa hecta 224.8 uliodumu zaidi ya miaka 10 sasa  ukihusisha wananchi wapatao 4000 kutoka Cha Simba, Chatembo, Chachui pamoja na Kiwanda cha Saruji cha Wazo na kuumaliza na kuingia makubalinao kwa wananchi wapatao 4,000 wa eneo hilo kulipa tozo ya primer

Eneo hilo ambalo thamani yake ni takribani shilingi bilioni 60 limekaliwa na wananchi kwa muda mrefu lilibadilishwa Juni 13, 2015 kutoka matumizi ya uchimbajji wa kukoto na mchanga na kuwa eneo la makazi.

Habari Zifananazo

Back to top button