RIPOTI MAALUM: Majeneza yatumika kuingiza bidhaa za magendo

Ng’ombe, punda vitendea kazi vikuu bandari bubu

WAKATI Serikali ipo kwenye mchakato wa kujenga Gati katika bandari ya Mbweni, uchunguzi umebaini kuwa wafanyabiashara wanaokwepa kodi wanatumia majeneza na magari ya mafuta kuingiza bidhaa za vipodozi, kanga, vitenge, betri na vyakula.

Uchunguzi huo ambao umefanywa katika bandari ya Mbweni na bandari bubu ya Kunduchi na Ununio jijini Dar es Salaam, umebaini kuwa majahazi na boti ndogo yanaingiza bidhaa hizo kutoka visiwa vya Zanzibar na wakati mwingine nchi jirani.

“Mbinu zipo nyingi wengine wanatumia jeneza unakuta limejazwa vipodozi, kanga au vitenge au bidhaa ndogo ndogo kama betri za tochi mtu akiona anaweza sema maiti, barabarani watu wakiona wanachukulia kawaida kuwa ni watu wamefiwa, ” HabariLeo imeelezwa.

Watoa taarifa mbalimbali katika uchunguzi huu uliofanyika kwa karibu mwezi mmoja waliozungumza na HabariLeo wamesema kuwa bandari ya Mbweni na Kunduchi inatumika kusafirisha dawa ya kulevya kutoka Zanzibar kuja Dar es Salaam na mafuta ya kupikia aina ya Korie na sabuni za unga.

Bidhaa hizo husafirishwa usiku na kusafirishwa kutoka ufukweni kwa kutumia ng’ombe na punda mpaka kwenye nyumba za kukodisha zilizoko kwenye Kijiji cha Mbweni, ambako huhifadhiwa.

Bidhaa hizo huchukuliwa usiku kwa kutumia magari na pikipiki kupelekwa maeneo mbalimbali ya jiji, lakini soko kubwa la bidhaa hizo lipo eneo la Manzese, wilaya ya Kinondoni na Kariakoo.

Serikali inatumia mbinu mbalimbali kutatua tatizo hilo ikiwepo kuanzisha doria ya Polisi na Mamlaka ya Mapato na hivi karibuni imewekwa kontena linalotumika kama ofisi ya TPA, Mamlaka ya Mapato, Wakala wa Vipimo na TBS.

Hata hivyo, magari ya kubeba magendo yanasemekana kuwa na mwendo mkali kuliko magari yanayotumika na TRA, makundi yanayoendesha magendo yanajua ratiba ya doria na hivyo kutumia wakati doria isipokuwepo kusafirisha bidhaa hizo kwenda Manzese na maeneo mengine jijini Dar es Salaam.

Mtoa habari mwingine amesema, “pamoja na ulinzi uliopo binadamu huwezi kuwazuia wakiamua lao, wana mbinu nyingi za kupitisha mizigo, unalinda Mbweni, Ununio, Msasani, Kunduchi, Kawe, Kigamboni bidhaa zinapitishwa kama kawaida.”

Hata hivyo, uchunguzi mwingine ambao HabariLeo umebaini kuwa mbali na kupitisha bidhaa kupitia bandari bubu, pia wafanyabiashara hao wamebuni njia nyingine ambayo ni kutumia magari ambayo tayari yameshusha mafuta na kupakiza bidhaa za magendo.

Bidhaa nyingi ambazo zimekuwa zikiingizwa nchini kinyemela ni vipodozi, sukari, mafuta ya kupikia, tairi, betri za tochi, maziwa ya unga, kanga na vitenge.

Magari ya kusafirisha nishati ya mafuta, baada ya kupakua nishati hiyo inaelezwa kuwa pia hujazwa vipodozi hususani visivyo na ubora ambavyo huingizwa kutokea nchini jirani, hali ambayo inaathiri utekelezaji wa kuwakinga watumiaji wa vipodozi visivyo na ubora.

Diwani wa Kata ya Mbweni Single Mtambalike, akizungumza na HabariLeo amesema: “Kwa kweli kwa sasa tuna Polisi Jamii, lakini pia kuna doria ya Mamlaka ya Mapato, Mbweni kwa sasa biashara ya magendo imedhibitiwa kwa kiasi kikubwa.

“Kama biadhaa zinapita basi zinapitishwa hapo hapo kwenye kijiji ambako kuna mamlaka zote, maana maeneo mengine hawawezi kwa vile kumezungukwa na kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), na Chuo cha Usalama wa Taifa, wote hao tunashirikiana nao katika kudhibiti biashara ya magendo.

“Kikubwa tu kwa sasa ni Bandari ya Mbweni iboreshwe iwe na miundombinu rafiki ikiwemo ya barabara ili meli kubwa za mizigo ziweze kushuka, ”amesema Mtambalike.

Kwa upande wa Diwani wa Kunduchi, Michael Urio akizungumzia hilo amesema changamoto kubwa iliyopo ni namna ya kudhibiti biashara hiyo ya magendo kupenya kwenye bandari bubu ukizingatia eneo hilo limezungukwa na bahari.

“Changamoto kubwa bidhaa zinapitishwa usiku, halafu wafanyabiashara hao sio watu wepesi wengine ni wazito, kuna muda mtu unatishiwa mpaka uhai wako, kuchomewa nyumba, nguvu yetu kama ‘local government’ ni ndogo,” amesema na kuongeza:

“Wakati mwingine vitendo vya rushwa kwa baadhi ya watendaji unakuta mnafanya doria mnakamata mtu na mapipa ya mafuta anajifanya kuuza kama maji, lakini cha kushangaa siku mbili kaachiwa yupo mtaani,” anasema.

Naye Mkazi wa Kunduchi, Samweli Julius anasema: “Bidhaa za magendo zinapitishwa usiku, tena wanaendesha magari kwa kasi sana, wana fujo wakati mwingine mpaka wanasababisha ajali, ni kero kubwa kwa kweli.

“Kingine doria ya Polisi ipo, TRA wapo, Polisi Jamii wapo kila mahali lakini bidhaa zinaingizwa kwa magendo, kuna maofisa ambao hawatimizi wajibu wao au kuna vitendo vya rushwa, kama vikosi vyote vipo na vinafanya kazi kwa weledi bidhaa sokoni zinafikaje? Alihoji.

Katika kikao cha Waziri Mkuu na wafanyabiashara kilichofanyika  Mei 17, 2023 uwanja wa Mnazimoja baada ya wafanyabiashara kugoma kufungua maduka kwa siku tatu wakilalamikia utitiri wa kodi, mmoja wa wafanyabiashara alisema “Vitenge sasa hivi ni sawa na dawa za kulevya, yani havipiti kokote kule…kontena zote za Vitenge sasa hivi zinakwenda Zambia,…tunarudi nyuma nyuma tunaviingiza tena nchini, TRA wakitubana sisi, na sisi tunaangalia mnyonge wetu serikali tunawaibia, Mheshimiwa Waziri Mkuu, au hamtaki wanawake wapendeze? Alihoji mmoja wa wafanyabiashara huyo

HabariLeo imezungumza na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo ambaye amekiri kuwa bidhaa za magendo bado zinaingizwa kwa wingi nchini licha ya udhibiti uliopo.

“Ni kweli bandari bubu zipo nyingi kutokana na kuwa na ukanda wa bahari wa kilomita takribani 1,400 kutoka Mtwara hadi Tanga, katika ukanda huo tuna bandari rasmi chache kama Mtwara, Lindi, Kilwa, tunayo Dar es Salaam, Bagamoyo lakini humo katikati kuna bandari nyingine bubu nyingi tu,” amesema Kayombo na kuongeza:

“Mizigo hushushwa kwa majahazi au boti ndogo ndogo na kuingizwa nchi kavu. Tuna vikosi vya doria vya nchi kavu maeneo mbalimbali, lakini tuna doria kupitia bahari.

“Lakini kama mnavyojua ukanda wa bahari ni mrefu si rahisi kuwa kila mahali, hivyo tunawategemea sana raia wema wanaotupa taarifa hasa inategemea na usahihi wa taarifa hizo.

“Wakati mwingine wafanyabiashara wana watu wao wanaowatumia kupeleleza wapi tupo ili wapitishe bidhaa kwa nyakati tofauti tofauti.

“Ili kukomesha tabia hii bidhaa ikikamatwa inataifishwa, chombo kilichobeba bidhaa hizo kinataifishwa na wakati mwingine hata tukibaini kuna nyumba ambayo imehifadhi bidhaa za magendo tunaitaifisha.

“Bidhaa zikikamatwa tunaruhusiwa kuinadi kama inafaa kwa matumizi kama sio ya kula, ila kama ni bidhaa ya kula inathibitishwa na taasisi nyingine TMDA na TBS wakithibitisha ubora wake basi tunaruhusiwa kunadi au tuitoe katika taasisi za serikali aidha ni shule za serikali au magereza, polisi kwa matumizi yao.

“Lengo ni kukata mtaji, ifahamike kwamba watu hawa wana mbinu nyingi na michoro mingi ya kufanya biashara kwa hiyo kuanzia Kigamboni kuna bandari bubu hizo, maeneo ya Msasani, Kunduchi, Mbezi Beach, Mbegani mpaka Bagamoyo…; biashara ngumu kuidhibiti lakini tunapambana.

“Hii shughuli hii ni haramu na watu wanaofanya ni haramu, na wenyewe wanatumia mbinu haramu kujilinda na wakati mwingine wanaweza kudhuru maisha ya watumishi wetu pale wanapojizatiti vizuri.

“Ukiachia mbali kudhibiti mapato, mipaka hii ambayo tunaisimamia tunashirikiana na vyombo vingine vya dola kudhibiti kuingiza bidhaa haramu, kama bidhaa za vyakula vinaingizwa kwa njia haramu basi hata dawa za kulevya, silaha nazo zinaingizwa kwa njia haramu,” anasema.

Kayombo, anataja madhara ya bidhaa hizo kuingia nchini mbali na upotevu wa mapato, madhara ya pili kwa kuwa hazijapita mikononi mwa taasisi zinazolinda bidhaa hivyo hazijathibitishwa kwa hiyo viwango hivyo havijulikani na vinaweza kuwa na madhara kwa watumiaji.

“Lakini pia kama mtu kaingiza bidhaa kwa magendo ataleta ushindani usio haki na kuuza kwa bei ya chini, wakati yule aliyelipa kodi atauza bei juu, na pia aliyeingiza bidhaa kwa magendo hakika hatotoa risiti…; “Ndio maana tunatoa elimu kwa wananchi, kuwa na uelewa mpana juu ya biashara ya magendo na kutoa taarifa,” anasema.

SERA YA TBS
Changamoto ya bidhaa zinazoingizwa kwa njia haramu si tu zinainyima nchi mapato, bali zinaweka hatarini maisha ya walaji kwani huwa hazikaguliwi na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lenye mamlaka ya kusimamia utekelezaji wa viwango kama ilivyoanishwa katika Sheria ya Viwango Tanzania ya Mwaka 2009.

Sheria hiyo inaipa TBS majukumu kadhaa ikiwemo kusaidia viwanda kuweka na kusimamia utekelezaji wa mifumo ya ubora; kutoa elimu kuhusu viwango; kukusanya, kuchapisha na kusambaza taarifa kuhusu viwango; na kupima ubora wa bidhaa zinazotoka nje ya nchi kabla hazijasafirishwa.

Pamoja na kuwepo kwa mamlaka hiyo, TBS yenyewe inakiri kuendelea kukamata bidhaa zisizokidhi viwango katika masoko.

Mathalan, Januari 14, mwaka huu, Kaimu Meneja wa TBS Kanda ya Mashariki, Francis Mapunda aliviambia vyombo vya habari kuwa bidhaa zisizokidhi viwango zilikamatwa baada ya kufanyika ukaguzi wa kushtukiza kwenye masoko yaliyopo kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro pamoja na Pwani.

Baadhi ya bidhaa zilizokamatwa na kuteketezwa ni pamoja na vipodozi, kofia za pikipiki ambazo ni tani 20 zenye thamani ya Shilingi milioni 400.

MADHARA KWA VIWANDA VYA NDANI
NIDA Textiles ni moja ya viwanda vya nguo hapa nchini ambavyo vimejikita katika uzalishaji wa kanga na vitenge. Mapema mwaka huu uongozi wa kiwanda hicho kilichopo nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, kiliwasilisha ombi kwa Serikali ya mkoa kudhibiti vitenge vinavyoingia sokoni kwa njia ya magendo na kuathiri uzalishaji.

Taarifa ya NIDA Textiles iliyowasilishwa na meneja wake, Mohamed Honelo ilibainisha kuwa uzalishaji kiwandani hapo umeshuka kutoka mita milioni 8 mpaka milioni 4, hiyo inaonesha kuwa kwa sasa kiwanda kinazalisha nusu tu ya uwezo wake, jambo lililomsukuma Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amosi Makalla kuiagiza Mamlaka ya Mapato (TRA) kupambana na hali hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button