Ripoti matumizi ya intaneti wanawake Kagera yazinduliwa

MASHIRIKA yasiyo ya kiserikali Omuka Hub  na Policy  wamezindua matokeo ya ripoti  inayoainisha uzoefu wa wanawake wa vijijini mkoani Kagera na changamoto zinazowakumba katika matumizi ya intaneti.

Uzinduzi huo ulikutanisha wawakilishi kutoka  Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Wizara ya Habari, Mawasiliano  na Teknolojia ya Habari, pamoja na baadhi ya wanawake kutoka  mkoani Kagera, kujadiliana kuhusu matokeo ya ripoti na kupanga mikakati ya pamoja.

Viongozi wa mashirika ya  Omuka Hub na Pollicy,  Dorice Kaijaga  na Navina Mutabazi, walieleza mbele ya wadau  kuhusu matokeo ya kampeni yao ya siku 16 ya utafiti na mafunzo ya ujuzi kidijitali kwa wanawake wa Mkoa wa Kagera, katika mkutano uliohudhuriwa pia na maofisa wa serikali na wadau jijini Dodoma.

Kampeni yao hiyo ilijikita katika mambo ya changamoto na manufaa ya matumizi ya mitandao, pia kuwaelimisha wanawake namna bora ya kutumia mitandao hiyo kuboresha biashara zao na kupata ujuzi wa mambo mbalimbali kupitia interneti.

Walieleza kuwa utafiti huo ulifanyika mkoani Kagera kwa siku 16 za kupinga ukatili, ambapo walikutanisha wanawake 80 waishio vijijini, wanawake hao walieleza changamoto mbalimbali zinazowakabili katika matumizi ya Intaneti pamoja na faida wanazozipata kupitia matumizi ya intaneti.

Baadhi ya wanawake waliowakilisha wenzao kutoka mkoani Kagera, walipata wasaa wa kuwasilisha taarifa ya kile walichokieleza, wakati mashirika haya yanafanya utafiti.

Miongoni mwa waliyoeleza ni changamoto ya upatikanaji wa mtandao wa intaneti kwa mikoa ya pembezoni, gharama za vifaa vya intaneti kuwa kubwa,  baadhi kukosa uhuru wa matumizi ya intaneti kutoka kwa waume zao, pamoja na gharama za vifurushi vya simu kuwa kubwa kuliko uwezo wao.

“Mkoa wa Kagera unakabiliwa na kutokuwepo mtandao wa kutosha wa intaneti, lakini bado wanawake wengi baadhi yao wanakumbana na ukinzani wa baadhi ya wanaume kutowaruhusu kumiliki simu zenye mitandao ya kijamiii kwa mawazo ya kusalitiwa.

“Kama wanawake tunatambua fursa na mafunzo yanayopatikana kupitia simu za mkononi na tunaomba mafunzo yanayohusu umuhimu wa matumizi ya intaneti yawahusishe pia wanaume, “Esther Goldian mwakilishi wa wanawake kutoka Kagera.

Asia Abdallah kutoka Wizara ya Habari, ametoa pongezi kwa mashirikia kuona fursa iliyopo kwa wanawake na namna mashirika hayo yanavyotoa elimu kwa wanawake wa mikoa ya pembezoni, jambo ambalo litawasaidia wanawake wengi kutangaza bidhaa zao kupitia simu za mkononi na kujifunza ujuzi mbalimbali kupitia intaneti.

Habari Zifananazo

Back to top button