MKURUGENZI na muaandaaji wa shindano maarufu la kusaka vipaji vya muziki, Bongo Star Search (BSS), Ritha Paulsen amemsifia msanii Rajabu Abdul ‘Harmonize’ kwa kutokata tamaa na kuonesha ushindani mpaka sasa licha ya wao kumkataa hajui kuimba kwenye mchujo wa BSS mwaka 2010.
Ritha ameeleza hayo Alhamis jijini Dar es Salaam akifafanua kwa namna alivyo Harmonize na aliyopitia amegundua siyo mtu wa kupewa moyo bali ni mtu wa kupokea changamoto ngumu na kuwathibitishia watu tofauti na vile wanavyowaza, akikiri hilo ndilo lililomfanya mpaka msanii huyo yupo hapo alipo sasa.
“Kiukweli kwanza katika watu waliomkataa siku ya usaili mimi sikusema chochote lakini siku ile hakufanya vizuri, yeye mwenyewe analijua hilo. Ni mtu ambaye alikuwa na ‘idea’ kwamba anajua na ni wale watu ambao labda asingeambiwa hajui asingekuwa huyu aliye leo, kuna watu wa aina hiyo kwamba huruma haiwasaidii.
“Na unaona mpaka sasa ushindani wake jinsi ulivyo, ni mtu ambaye mshindani, ana mikwaruzo ya hapa na pale na anazidi kusonga, ni aina ya mtu mpambanaji wa mtindo huo, anataka kuonesha tofauti na unavyowaza ndiyo maana tulipomwondoa hakuibuka mwisho wa mwezi ule, ilimchukua miaka mitano akaja kutokea lakini siku ile yeye mwenyewe anajua hakufanya vizuri…
“Unajua wapo watu wanafeli mwanzo, mtu anafeli darasa la saba lakini anakuja kuwa na ‘ma-degree’ na ‘ma-PhD’ na huyu (Harmonize) angenitusi au kunisema vibaya kwenye nyimbo zake ningemuelewa labda sababu ana hasira kwamba tulimkatalia lakini alifanya tofauti. Alituimba mimi na Master (Jay) kwamba tulimfanya hasira zizidi, namuelewa kwa sababu hata mimi kuna muda nipo hivyo nataka nikuoneshe kuhusu ‘challenge’ unayonipa,” alisema Ritha.
Aidha, hivi karibuni Harmonize alipokuwa akitumbuiza Dodoma, alimuita jukwaani Ritha na kumuonesha ishara ya kuheshimu kwa kile anachokifanya, akisisitiza hakuna tofauti kati yao kwa kuelewa mchango wake katika muziki, tukio ambalo Ritha anasema lilimshtua na kumpa uwoga mno lakini baadaye alitambua vizuri nguvu ya ushindani aliyonayo Harmonize moyoni mwake na ndiyo maana mpaka leo anashindana na watu wakubwa.